Beki Juma Abdul, Yondani waongeza nguvu Yanga

Wednesday September 11 2019

 

By Mbushi Kwilasa

Mwanza. Beki wa Yanga, Juma Abdul aliyekuwa amefiwa na mama yake leo ameungana na wenzake katika mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja Nyamagana, Mwanza.

Yanga ipo kambini Mwanza kujianda na mchezo wake wa kusaka kufuzu kwa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zesco ya Zambia utakaochezwa September 14, kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Beki Abdul aliondoka kambini hapo kufuatia msiba wa mama yake mzazi uliotokea wiki moja iliyopita, leo ameungana na wenzake mazoezini  kujiandaa na mchezo huo.

Mbali na nahodha huyo msaidizi, wachezaji wengine walioungana na timu leo kwenye mazoezi ya mwisho kwenye kambi ya Mwanza ni kiungo Mohamed Issa na Kelvin Yondani waliokuwa katika kikosi cha Taifa Stars kilichocheza dhidi ya Burundi.

Wachezaji wanne hawajafanya mazoezi ya leo ambao ni Kipa Farouk Shikhalo (Kenya)  na Patrick Sibomana (Rwanda) pamoja na Paul Godfrey na Issa Bigrimana ambao ni majeraha.

Yanga imefanya mazoezi yake ya mwisho jijini Mwanza kabla ya kupanda ndege leo jioni kurudi Dar es Salaam tayari kuwavaa Zesco katika mchezo wa Ligi ya mabingwa Afrika.

Advertisement

Advertisement