Arsenal lazima ipasue Ulaya

Thursday June 13 2019

 

KOCHA Unai Emery ameripotiwa kuwa na Pauni 40 milioni tu kwenye bajeti yake ya usajili wa majira haya ya kiangazi huko Ulaya.

Bajeti hiyo inazua maswali mengi, ataweza kuunda kikosi cha aina gani kitakachokuwa na uwezo wa kushindania mataji msimu ujao na kubwa zaidi kurejea kwenye mchakamchaka wa Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kushindwa kufanya hivyo kwa misimu mitatu mfululizo.

Hata hivyo, kikosi cha Arsenal kinahitaji marekebisho kidogo tu, ambayo kama Kocha Emery atacheza karata zake sawa, basi ataunda timu itakayokuwa tishio kwenye Ligi Kuu England na pengine kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2020/21.

Kikosi hicho cha Emirates huko Emirates, tayari kina mastaa wa maana kama Pierre-Emerick Aubameyang, Alexandre Lacazette, Mesut Ozil, Lucas Torreira, Matteo Guendouzi na wengineo, ambao atahitaji kuwabakiza kwenye timu ili aongeze wengine wachache tu kuifanya timu hiyo kuwa moto wa kuotea mbali.

Vita pekee ambayo inamkabili Emery ni kuhakikisha wakali hao wanabaki baada ya kudaiwa kusakwa na timu mbalimbali, ambapo Aubameyang anawindwa huko China, Lacazette Barcelona na Torreira huko Italia.

Emery hapaswi kuruhusu staa yeyote aondoke kwenye orodha hiyo hasa kutokana na bajeti yake aliyokuwa nayo ya Pauni 40 milioni.

Advertisement

Lakini Emery akiwa mjanja anaweza kunasa huduma bora bure kabisa kutoka kwa mastaa wa maana ambao wakitua tu kwenye kikosi chake suala la kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya na kutamba kwenye Ligi Kuu England ni la lazima.

Emery anaweza kuzipata bure kabisa huduma za mastaa hawa; Mario Balotelli, Hatem Ben Arfa, Yacine Brahimi, Gary Cahill, Andy Carroll, Matteo Darmian, Alan Dzagoev, Diego Godin, Hector Herrera, Max Kruse, Filipe Luis, na Juan Mata.

Wengine ni James Milner, Alberto Moreno, Samir Nasri, Adrien Rabiot, Franck Ribery, Arjen Robben, Daniel Sturridge na Antonio Valencia, ambapo kazi yake itakuwa kuwalipa mishahara tu na si pesa za kuwasajili.

Kwenye orodha za wachezaji hao, Emery anaweza kuchagua majembe machache tu. Baasi.

Advertisement