Hans Poppe, Manara waitwa Kamati ya Maadili

Friday August 14 2020

 

By Mwandishi Wetu

MJUMBE wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Zakaria Hans Poppe, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba, Hajji Manara na mchezaji Bernard Morriso wamepelekwa kwenye Kamati ya Maadili ya shirikisho hilo kwa madai ya kutoa vitisho.

Malalamiko hayo yametolewa na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji kupitia Mwenyekiti wake, ambapo wanalalamikiwa wanafamilia hao wa soka kuchochea hisia za jamii na kutoa vitisho kuhusu shauri lililokuwa mbele yake.

Juzi Jumatano, Kamati hiyo ilitangaza ramsi ushindi wa Morrison juu ya shauri lake alilokuwa amepeleka kwenye kamati hiyo kuhusu Yanga kughushi mkataba wake mpya ambapo uamuzi ulitolewa kwamba mkataba wake ulikuwa na mapungufu hivyo anaruhusiwa kucheza timu yoyote.

Hata hivyo, Morrison baada ya maamuzi hayo alipelekwa Kamati ya Maadili kwa kosa la kusaini mkataba mwingine Simba wakati shauri lake lilikuwa linaendelea hivyo haya ni madai yake ya pili kwenye kamati hiyo.

Katika taarifa hiyo iliyotolewa na Ofisa Habari na Mawasiliano TFF, Cliford Ndimbo inaeleza kuwa Sekretarieti yao imempeleka Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga, Hassan Bumbuli katika Kamati ya Maadili kwa kutoa taarifa za uongo.

"Wahusika watapewa malalamiko dhidi yao kwa njia ya maandishi na mwito wa kuhudhuria kikao cha Kamati ya Maadili," imeeleza taarifa hiyo.

Advertisement

Advertisement