Yakub hana presha Azam

Muktasari:

Yakub aliondoka nchini na kurejea Ghana baada ya Ligi kusimama wakati ugonjwa wa COVID 19 kuanza kusambaa kwa kasi nchi mbalimbali.

THOMAS NG'ITU

BEKI wa Azam FC, Yakub Mohamed amesema licha ya kukosekana katika mazoezi ya timu yake yalioanza wiki hii wakijiandaa na msimu ujao wa Ligi Kuu Bara, anaamini ana nafasi kikosi cha kwanza.

Yakub aliondoka nchini na kurejea Ghana mwishoni mwa mwezi Februari baada ya ligi kusimama wakati ugonjwa wa Covid-19 kuanza kusambaa kwa kasi nchi mbalimbali na tangu hapo hajarejea.

Akizungumza na Mwanaspoti leo Ijumaa Agosti 07, 2020 akiwa nyumbani kwao Ghana, amesema anaendelea kufanya mazoezi kama kawaida ili kujiweka fiti.

"Sijaacha kufanya mazoezi hata kidogo, niko fiti na naendelea kuwa fiti nina amini namba yangu ipo na hilo sina wasiwasi nalo kabisa kwa sababu nafanya mazoezi,".

Yakub amesema mwezi huu anaweza kurejea nchini kama tu viwanja vya ndege vitakuwa vimefunguliwa kwani tangu mlipuko wa ugonjwa huo utokee nchi nyingi walizuia usafiri wa anga.

Beki huyo amekuwa muhimili mkubwa katika safu ya ulinzi akicheza sambamba na Agrey Morris, kukosekana kwake na Morris aliyekuwa anasumbuliwa na majeraha, nafasi zao zilichukuliwa na Oscar Masai pamoja na Abdallah Kheri.