Kocha mpya Yanga atanguliza kiungo, straika

Muktasari:

MWANASPOTI linajua kwamba kocha mpya msaidizi wa Yanga, Mecky Mexime (sasa Kocha msaidizi wa Kagera) atasaini mkataba wiki ijayo lakini amemtanguliza kiungo fundi, Zawadi Peter Mauya.

MWANASPOTI linajua kwamba kocha mpya msaidizi wa Yanga, Mecky Mexime (sasa Kocha msaidizi wa Kagera) atasaini mkataba wiki ijayo lakini amemtanguliza kiungo fundi, Zawadi Peter Mauya.

Mauya ambaye msimu uliopita aling’ara na Kagera Sugar tayari yupo Jijini Dar es Salaam na jana mchana alipiga pilau ya Sikukuu ya Eid el Hadj na mabosi wa Yanga na jioni alitarajiwa kusaini mkataba wa miaka miwili.

Lakini vilevile Mwanaspoti limejiridhisha kwamba beki kisiki wa Coastal Union na Taifa Stars, Bakary Mwamnyeto jana amesaini miaka miwili Yanga, hukupia straika wa Kagera Sugar, Yusuf Mhilu akitarajiwa kumwaga wino Jangwani wiki ijayo.

Mwamnyeto ambaye pia Simba walikuwa wakimuwania alitua Jijini Dar es Salaam juzi Alhamisi jioni na usiku wake alikuwa na viongozi wa Yanga mitaa ya Sinza kabla ya jana kukubaliana na kusaini mbele ya wakala wake Kassa Musa.

Usajili wa Mwamnyeto umeinufaisha Coastal kwani miongoni mwa makubaliano ni kwamba GSM itawapa udhamini wa miaka miwili usiopungua Sh70milioni.

Kuhusu Usajili wa Mauya, Mwanaspoti linajua kwamba umekamilika jana huku mabosi wa klabu hiyo wakifanya siri nzito lengo likiwa ni kutambulisha mastaa wao wapya katika wiki ya mwananchi ambayo ni sherehe ya klabu hiyo.

Mauya (pichani katikati) ambaye anacheza nafasi ya kiungo mkabaji anasifika na ujuzi wa kukaba na kupambana akiwa dimba la chini lakini pia akiwa na ubora wa kucheza kama kiungo mchezeshaji.

Mauya msimu uliopita aliwahi kuamsha zogo baada ya kumpiga mabuti Ibrahim Ajibu wakati Kagera Sugar ikicheza na Simba kule Kaitaba kisha msala huo kuvuma lakini baadaye wawili hao wakaombana radhi na maisha yakaendelea.

Habari za uhakika kutoka ndani ya Yanga ni kwamba dili la Mhilu limeiva atarejea katika klabu yake hiyo ya zamani na tayari ameshapewa mkataba ambao atasaini muda wowote ikiwa ni pendekezo la Mexime,

 

Dili la Maxime

Ingawa jana ilisambaa picha ya kipa namba tatu wa Kagera, Ramadhani Chalamanda akiwa na mkataba wa Yanga, lakini uhakika ni kwamba Maxime amemtanguliza Mauya. Chalamanda alimuomba Mauya mkataba huo auzie sura tu ila hayumo kwenye rada za Yanga.

Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti iliwahi kuandika pia miezi kadhaa iliyopita ni kwamba Maxime atasaini Yanga keshokutwa Jumatatu kuchukua nafasi ya Mkwasa.