Shilole star wa pili kuanika vipigo anavyopata kwenye mahusiano yake

Wednesday July 8 2020

 

By Imani Makongoro na Nasra Abdallah

Dar es Salaam. Msanii, Zuwena Mohammed (Shilole) amewaomba radhi mashabiki wake kwa kudanganya kuhusu ndoa yake.

Shilole aliyeolewa miaka kadhaa iliyopita na Uchebe amesema amekuwa mtu wa kuambulia vipigo kwenye ndoa hiyo.

Katika ukurasa wake wa Instagram, Shilole ameposti picha akiwa ana majeraha usoni huku akiandika namna ndoa yake hiyo ilivyo na machungu.

Shilole anafunguka hayo ikiwa imepita miezi kadhaa tangu msanii mwingine wa bongo Fleva, Ruby kueleza namna alivyokuwa anavumilia vipigo vya mpenzi wake Kusah.

Ujumbe wa Shilole umesomeka hivi; Naandika haya, nikiwa na akili timamu na utulivu, la kwanza kabisa nataka kuomba radhi jamii yangu. Naomba radhi kwa sababu niliwaaminisha ndoa yangu haina tatizo, huku ukweli ukiwa hauko hivyo, nimekuwa mtu wa kuambulia vipigo na mengine yasiyozungumzika, Naomba radhi kwa sababu niliposikia wanawake wenzangu wakipigwa niliwaambia pazeni sauti, niliposikia mwanamke kule Kigamboni ameuwawa na kuchomwa moto niliomboleza na jamii na kusema Bora angesema… huku mimi nikijikausha na kujitoa kwenye kundi lao wakati ukweli wangu mimi ni mwenzao, Naomba radhi.”

Mimi ni kioo cha jamii, tena sura kubwa ya wanawake. Leo nimeona nivunje ukimya kwa kuweka wazi kwamba mume wangu Ashrafu Sadiki, maarufu kama Uchebe amekuwa ananipiga saaana, na tena hata baada ya kunipiga hajali kupiga simu wala kujua naendeleaje, nauguzwa na watu baki hospitali, na bado manyanyaso mengine yanayoikosesha hii ninayoiita ndoa uhai na furaha

Advertisement

Na zaidi nina watoto, watoto wanaoniangalia kama Baba na Mama, leo nikubali kufa na kuacha wanangu barabarani, sitaweza.

'Uchebe' ni mwanaume niliyempenda, nilimvumilia kwa madhaifu yote, nikampa kila kitu, (Utu wangu, Mali Zangu na hata palipotakiwa kumuendeleza asimame mwenyewe nilifanya kwakuwa nilijua tuko pamoja), lakini hilo halikuwahi kuzuia vipigo, dharau na usaliti.

Siku mbili zilizopita baada ya kutoka sabasaba kutafutia watoto wangu na kumtafutia yeye nilipigwa sana. sababu za kupigwa ni migogoro midogo ya kawaida ambayo ipo kwenye kila ndoa, sio kwamba amenifumania au mambo yanayoshindwa kuzungumzika, hapana, Tena Namuheshimu sana, lakini solution aliyoiona ni kunipiga kinyama bila huruma, tena kwa kunishtua na ngumi nikiwa usingizini, Kama mnavyoona picha hapo ni matukio ya siku tofauti tofauti.

Najua nitalaumiwa kwa kuweka hili mtandaoni, ila sina namna, maisha yangu ni maisha ya watu kwa kiasi kikubwa, jamii inanitazama kama mfano. Nimefika mwisho, na kuanzia sasa naomba nisitambulike kama Mke wa Uchebe, ila Mama alieamua kuweka maslahi ya watoto wake mbele na kuamua kuwa mwenyewe kwa usalama na furaha yake

Wakati nahangaikia mambo yangu ya ndoa, post hii itumike kuwakumbusha wanawake tuvunje ukimya, tupinge ukatili, tutakuja kuuliwa sababu," alimaliza Shilole.

Wasanii mbalimbali wamempa pole Shilole katika ukurasa wake huo kwa hicho alichoeleza akiwemo Linah Sanga ambaye aliandika chini ya ujumbe alioundika Shilole wakuelezea namna alivyokuwa akipigwa na mme wake, kwamba yeye aliamua kuyaepuka hayo mapema.

Advertisement