Bosi mpya Simba kutembeza panga kambi yahamishwa

Tuesday October 1 2019

Mwanaspoti, Bosi mpya Simba, Tanzania, kutembeza panga Afrika Kusini

 

Dar es Salaam. WAKATI Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ akiendelea kuboresha klabu hiyo ndani ya uwanja na nje, mambo yameanza kushika kasi baada ya Mtendaji Mkuu, Senzo Mazingisa kuibuka na mikakati mbalimbali ikiwemo kubana matumizi.
Mazingisa, ambaye alisafiri na timu yake kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa wala hakulaza damu baada ya kuitisha kikao maalumu na watendaji walio chini yake akizungumza na kila mmoja kuhusu mikakati yake ya utendaji kazi.
Habari za kuaminika zinaeleza, kabla ya kukwea pipa kwenda mikoa ya Kagera na baadaye Mara, Mazingisa alikutana na kuzungumza na watendaji hao wakiwemo wapya walioajiriwa hivi karibuni kila mmoja kwa nafasi yake.
Katika mazungumzo hayo ambayo Mwanaspoti limeyanasa, Mazingisa alitaka kufahamu malengo ya muda mrefu na mfupi ya kila mmoja kulingana na majukumu na nafasi yake ndani ya klabu hiyo na namna bora ya kuyatekeleza.

KUPUNGUZA BAJETI
Mwanaspoti limedokezwa katika maeneo ambayo Mazingisa anataka kuanza kuyafanyia kazi ni kupunguza gharama za matumizi kwa kukata maeneo ambayo hayana ulazima wa matumizi makubwa ya fedha.
Mmoja wa kigogo ndani ya Simba, ameliambia Mwanaspoti kuwa, Mazingisa anataka kabla ya mwaka huu kumalizika Simba iwe imeanza kuutumia uwanja wake wa mazoezi ili kuachana na utaratibu wa kukodisha viwanja.
Pia, amepanga kuangalia viwango vya mishahara ya wachezaji na gharama zingine ambazo sio za lazima ndani ya klabu.
“Hapo kupunguza gharama ndani ya kikosi Mazingisa alionekana kushangaa timu kama Simba kuwa na wachezaji kutoka Brazil.
“Mazingisa alisema kwa mahitaji ya soka la Tanzania au Afrika kwa jumla aina ya wachezaji kutoka mataifa ya jirani na hili ni moja ya eneo ambalo litaangaliwa kwa undani kuanzia sasa,” alisema mmoja wa watu wa ndani wa Simba.
Katika usajili wake wa msimu huu, Simba imewanasa Wabrazili watatu, Tairone dos Santos ambaye anacheza nafasi ya kiungo, Gerson Fraga (beki) na straika Wilker da Silva.
Usajili wa Wabrazil hao ulizusha gumzo kubwa kutokana na kutumia muda mwingi wakiwa benchi huku wakishindwa kuisaidia Simba kutamba kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo majeruhi.
Hata hivyo, Mwanaspoti linafahamu kuwa usajili wa wachezaji hao wa Kibrazili kila mmoja ameigharimu Simba kiasi cha kati ya dola za Marekani 30,000 hadi 40,000 (Sh 66milioni hadi 78 milioni) huku mishahara yao ikiwa ni dola 3,500 kwa mwezi (Sh7.8 milioni).

WAHAMA KAMBI
Katika kuhakikisha Simba inapunguza gharama kwenye kikosi chake, msimu uliopita wachezaji walikuwa wakiweka kambi kwenye hoteli ya Sea Scape ambayo kwa gharama ya kawaida kwa siku chumba kimoja thamani yake ni Sh 280,000.
Gharama hiyo ni pamoja na kifungua kinywa jambo ambalo uongozi wa Simba ulilazimika kuwa ma pishi wao Samuel Syprian, ambaye alikuwa anawapikia chakula wachezaji na benchi la ufundi.
Mbali ya gharama hiyo makocha Patrick Aussems na msaidizi wake Adel Zrane pamoja na baadhi ya wachezaji ambao, hawakuwa wamepatiwa nyumba za kuishi walikuwa wakiishi hotelini hapo kwa gharama ile ile hata wakati timu isipokuwa kambini.
“Mazingisa alikuja alikuta tayari uongozi umeshaingia makubaliano ya mwaka mmoja na hosteli ambazo zipo Mbweni jeshini kule ndani licha ya kuwepo malalamiko kwa baadhi ya wachezaji kutaka warudishwe Sea Scape, lakini amesisitiza kambi itabaki huko huko.
“CEO ametaka kambi ibaki Bweni na wachezaji wasirudi hotelini, ameridhishwa na mazingira kwa kuwa ni mwafaka kwa timu. Kuna utulivu wa kutosha,” alisema mtu huyo wa ndani wa Simba, ambaye aliomba jina lake lisiwekwe wazi gazetini kwa sababu za kiusalama.

UWANJA
Mwezi Oktoba kikosi cha Simba kitakwenda kutumia uwanja wake wa Bunju Complex, katika mazoezi yake ya kila siku na baadhi ya mechi za kirafiki wakati wa mapumziko ya ligi.
Katika kuhakikisha hilo linakamilika kwa haraka Mo Dewji pamoja na Aussems kila mmoja alitembelea ujenzi huo ambao uko hatua za mwisho na kusisitiza ukamilike haraka.
Simba ikihamia kwenye uwanja wake huo wataokoa zaidi ya Sh54 milioni ambayo hutumia kwa mwaka katika kukodisha viwanja vya kufanyia mazoezi.
Kwa kawaida Simba hutumia Sh500,000 kukodisha uwanja wa Gymkhana kwa ajili ya mazoezi huku ikitumia Sh300,000 kwa uwanja wa Boko Veterans kwa siku.
Mratibu wa Simba Abbas Selemani alisema ukiachana na pesa hizo ambazo wanalipa kwenye viwanja vya Gymkhana na Boko Veterans, pia hutumia fedha kukodi viwanja vya mikoani wanapokwenda kucheza mechi.
“Katika viwanja vya mkoani tunaweza kulipia si chini ya Sh100,000 ambayo kwa msimu mzima pamoja na vile ambavyo tunatumia kufanyia mazoezi Dar es Salaam, tunalipa kwa mwaka kama Sh54 milioni kwa maana hiyo kama uwanja wetu wa Bunju Complex utakamilika utapunguza gharama hii kubwa,” alisema Selemani.

SENZO HUYU HAPA
Kwa upande wake, Mazingisa alisema kwa sasa klabu hiyo ipo katika mpango wa kupunguza baadhi ya matumizi ili kuendana na bajeti na kufikia malengo ya msimu huu.
Bosi huyo ambaye ameambatana na timu Kanda ya Ziwa, juzi ilikuwa akifuatilia mazoezi ya timu yake kwenye Uwanja wa CCM Kirumba na Simba iliweka kambi kabla ya kutua mkoani Mara kumalizana na Biashara United.
Akizungumza jijini hapa, Mazingisa alisema taasisi yoyote huwa na mipango yake, hivyo Simba wameweka mikakati yao na ili kuitimiza lazima wapunguze baadhi ya vitu ili kuendana na bajeti yake.
Alisema licha ya wachezaji wa kigeni kutumia gharama kubwa, lakini ishu ya kutambua kama mchezaji fulani anatumia fedha nyingi kuliko wengine haina ukweli.
“Kampuni au taasisi huwa na malengo yake kulingana na bajeti, kwa hiyo hata Simba tupo kwenye mpango wa kupunguza gharama ili kuendana na bajeti,” alisema na kuongeza:
“Ni kweli wachezaji wa kigeni wanatumia bajeti kubwa, lakini mmoja huwa na majukumu na makubaliano yake na uongozi. Kila mmoja ana mkataba wake hivyo, wachezaji wote wapo sawa,” alisema kiongozi huyo.
Hata hivyo, alisema kabla ya jambo lolote kufanyika, Bodi ya Wakurugenzi hukaa na kujadili kwa masilahi mapana ya timu na baadaye hufanyiwa maamuzi.
Hata hivyo, kigogo huyo hakusita kupongeza kiwango cha wachezaji na matokeo waliyoyapata katika mechi tatu huku akisema Simba ina malengo makubwa kwenye medani za soka.
Alisema kwa mwenendo walionao Simba kwa sasa ni dhahili uwezekano wa kubeba tena ubingwa upo na kuwaomba mashabiki kuendelea kufurika viwanjani timu inapocheza.
“Kwa ujumla lazima niwapongeze wachezaji na benchi la ufundi, nilishuhudia mechi yetu na Kagera Sugar nilifurahia kiwango cha timu na matokeo yake na mwitiko wa mashabiki,” alisema Mazingisa.

Advertisement