Simba kaweza, kwa Yanga hii inakwama wapi

Muktasari:

Zahera, ambaye alianza michuano hiyo hatua ya awali kwa sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya Township Rollers ya Botswana kisha kwenda kupata ushindi wa bao 1-0 kule jijini Gaborone, Botswana na kusonga mbele.

YANGA iko kwenye mazoezi makali kujiandaa na mchezo wake wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zesco United ya Zambia, lakini kocha wake Mwinyi Zahera ameibuka na matumaini mapya kabisa ya kushinda na kusonga mbele.
Zahera, ambaye alianza michuano hiyo hatua ya awali kwa sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya Township Rollers ya Botswana kisha kwenda kupata ushindi wa bao 1-0 kule jijini Gaborone, Botswana na kusonga mbele.
Lakini, licha ya mechi ya Zesco United inayonolewa na kocha wa zamani wa Yanga, George Lwandamina, kutajwa utakuwa mgumu kutokana na ubora wa kikosi cha WAzambia hao, Zahera amefunguka haoni dalili za wapinzani wao kupona kabisa.
Akizungumza na Mwanaspoti, Zahera amesema kama Simba ilizichapa klabu bora za Al Ahly ya Misri na AS Vita ya Congo basi hakuna sababu ya mashabiki wa Yanga kuwa na hofu kwani, ushindi ni lazima.
Alisema licha ya Ligi Kuu ya Zambia kuwa bora na hata rekodi za nchi hiyo kisoka kuwa juu ya Tanzania, hilo haliwafanyi kuingia kinyonge kwenye mchezo huo kwa kuwa, wana kikosi bora msimu huu kinachoweza kupata matokeo mazuri bila kujali wanacheza nyumbani ama ugenini.
Yanga itaanza kukipiga na Zesco United Septemba 14, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaaam.
Kama Yanga itapata matokeo mazuri kwenye mechi zote mbili dhidi ya Zesco United itatinga moja kwa moja hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika viwango vya Fifa, Zambia iko nafasi ya 81 wakati Tanzania inashika nafasi ya 137.
“Mpira wa Congo, Misri na Algeria ni mkubwa kuliko Tanzania lakini Simba waliipiga Al Ahly, JS Saoura na AS Vita tena kwa mabao mengi, sasa Yanga tutashindwaje kuifunga Zesco?.
“Msimu uliopita katika michuano hii ya Afrika, Simba iliichapa JS Saoura ya Algeria mabao 3-0, iliifunga Al Ahly ya Misri bao 1-0 kisha ikaichapa AS Vita ya Congo mabao 2-1 na kutinga hatua ya makundi.
“Hivi sasa tofauti ya mpira baina ya nchi na nchi sio kubwa, Zambia kuwa ligi bora hakutufanyi tuiogope Zesco. Tutacheza mechi tukiwa na lengo moja la ushindi na lazima tuhakikishe linatimia,” alisema Zahera.
Alisema hana hofu na mechi hiyo licha ya Lwandamina kuifahamu Yanga kwa undani pamoja na staili ya soka lake.
“Hata kama Lwandamina alipita Yanga hakuna tatizo wala hatuna hofu kwani, mpira unabadilika sana. Hivi sasa tunaangalia Yanga hii dhidi ya Zesco, wao wana mipango yao na sisi tuna mipango yetu hivyo tutakutana uwanjani,” alisema Zahera.

Lwandamina aitega Yanga
Wakati Zahera akitamka kuwa Lwandamina huenda anaifahamu vizuri Yanga kwa sababu aliifundisha miaka ya nyuma, lakini Mzambia huyo amedai kutoifahamu na wala kutoifuatilia kabisa timu yake hiyo ya zamani na yuko bize na kukisuka kikosi chake.
Lwandamina alisema: “Nipo Zambia na sifuatilii kabisa nini kinaendelea huko Yanga kuelekea mechi yetu, sio muda wote ninakua naangalia mpira tu na hiyo sio kwa Afrika bali popote.
“Sikuwa nafahamu soka la Tanzania, Yanga pia niliifahamu baada ya kujiunga nayo na kuifundisha na sio kitu kingine,” alisema.
Kuhusu mshambuliaji wake wa zamani ambaye hivi sasa yupo Yanga, Maybin Kalengo, alisema hawezi kumzungumzi mchezaji huyo kwani, hayupo mikononi mwake kwa sasa.
Wakati Lwandamina akiipa kisogo Yanga kwamba hawafuatulii, Yanga nao wamejikita kujifua zaidi ambapo wanatarajia kuweka kambi ya wiki mbili jijini Mwanza kuanzia Septemba 4, mwaka huu na ikiwa huko itacheza mechi mbili za kirafiki.