Simba, Yanga zapewa tano kujitoa Kombe la Kagame

Tuesday June 11 2019

 

By Thomas Ng’itu

Dar es Salaam.  Muda mfupi baada ya Yanga kutangaza kujitoa kushiriki michuano ya Kombe la Kagame, wadau wa michezo wametoa maoni tofauti kuhusu uamuzi huo.

Yanga imeungana na Simba kutoshiriki michuano ya Kombe la Kagame iliyopangwa kuanza Juni 7 Jijini Kigali, Rwanda.

Wakati Simba na Yanga zikitangaza kujitoa, mabingwa watetezi Azam wamesema watakwenda Kigali kutetea ubingwa wao.

Mtendaji Mkuu wa Azam, Abdulkarim ‘Popat’ Amin alisema timu hiyo inatarajiwa kuondoka nchini Juni 6 kwenda Rwanda.

Kauli za wadau

Miongoni mwa wadau walitoa maoni baada ya Yanga kutangaza kujitoa katika michuano hiyo ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah.

Advertisement

Osiah alisema Simba na Yanga zimejitoa kushiriki Kombe la Kagame kwa kuwa zina mtazamo kwamba lazima zipeleke timu za kikosi cha kwanza katika michuano hiyo.

“Simba na Yanga wanawaza muda wote vikosi vya kwanza kuliko kikosi kwa ujumla, nadhani mashindano haya yangewajumuisha wachezaji vijana waliopanda au wale wasiocheza kabisa kwenda kushiriki,” alisema Osiah.

Alisema mashindano hayo yana manufaa kwa ngazi ya klabu na alitoa mfano kwa nchi za Uganda, Kenya na Burundi ambazo zitapeleka timu zao.

 “Timu zetu hazitashiriki lakini Uganda, Kenya, Burundi watakwenda na sisi tutasajili wachezaji kutoka hapo hapo katika mashindano hayo, hivyo yana umuhimu wake,”alisema Osiah.

Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Simba, Ismail Rage alidai viongozi wote wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) wanapaswa kujizulu kwa kushindwa kusimamia vyema mashindano hayo.

“Miaka ya 1973 na 1974 mashindano haya  yalianzishwa maalumu kwa ajili ya kujiandaa na klabu bingwa, lakini hivi sasa imekuwa tofauti. Naunga mkono Simba na Yanga kujiondoa,” alisema Rage.

Katibu Mkuu wa zamani wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Kanali Mstaafu Idd Kipingu alisema anashangaa Cecafa haina mawasiliano ya karibu na wanachama wake.

“Sijui kwanini Cecafa hawana mawasiliano mazuri na wanachama wake, wachezaji wametoka katika ligi wanatakiwa wapumzike,  najua timu zina wachezaji wengi lakini mawasiliano hakuna, hivyo nashauri kuwe na mawasiliano ya karibu

 “Mashindano haya ni mazuri kwa wachezaji kujijenga, kujiamini na kwa upande wa timu wangetumia kama mazoezi kwa ajili ya msimu ujao, lakini hili la Cecafa kutaka wachezaji 11 wa kikosi cha kwanza litazidi kuwagharimu wachezaji wanahitaji kupumzika,”alisema Kipingu.

Katika taarifa yake, Yanga ilidai haitashiriki mashindano ya msimu huu kwa kuwa idadi kubwa ya wachezaji wame wamemaliza mikataba na wengine wapo na Taifa Stars nchini Misri kwa Fainali za AFCON.

Juni 2, mwaka huu Cecafa iliwaandikia Yanga barua ya mwaliko ikiomba washiriki mashindano ya msimu huu.

Musonye

Katibu mkuu wa Cecafa, Nicholas Musonye alisema atawasiliana na TFF ili kupata barua zilizoandikwa na Simba, Yanga kujitia katika michuano hiyo.

"Kukosekana kwa Simba na Yanga siyo shida mashindano yatafanyika na yako palepale. Baada ya kupata barua rasmi kutoka TFF, ndio nitatoa tamko rasmi juu ya hilo," alisema Musonye.

Advertisement