Kenya yapata pigo, Mandela aumia mazoezini, kuikosa DR Congo

Monday June 10 2019

Mwanaspoti, Kenya, Mandela, aumia, mazoezini, DR Congo, Afcon, Stars

 

By Fadhili Athumani

Nairobi. Baada ya kupata ushindi wa 1-0, dhidi ya Madagascar Juni 7, Ijumaa timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars, inajiandaa kukabiliana na DR Congo katika mchezo wa pili wa kujipima nguvu, utakaopigwa Juni 15, Jijini Madrid, Hispania.

Kwa bahati mbaya sana, Stars, iliyoweka kambi ya wiki tatu, Jijini Paris Ufaransa, kwa ajili ya kujiandaa na fainali za Mataifa ya Afrika, AFCON 2019, itacheza na DR Congo, bila ya huduma za beki Brian Mandela.

Mandela, anayeichezea klabu ya Maritzberg United ya Afrika Kusini, ambaye ni beki wa kati na pacha wa Musa Muhammed, aliumia goti katika mazoezi ya Stars, leo asubuhi, na kwa mujibu wa taarifa ya madaktari wa timu, huenda akazikosa fainali za AFCON.

Akitoa ripoti ya athari ya jeraha, Kocha mkuu wa Stars, Mfaransa Sebastien Migne, alisema ripoti ya madaktari inaonesha kuwa itachukua muda mrefu kwa beki huyo kupona, lakini akasisitiza kuwa mbadala wake yupo.

“Brian aliumia goti mazoezini leo asubuhi, ripoti inaonesha itachukua muda kupona. Ni mmoja wa wachezaji wetu muhimu sana, habari mbaya zaidi ni kuwa atakosa fainali za mwaka huu," alisema Migne.

Aidha, Migne pia alidokeza kuwa, Nahodha msaidizi wa Stars, Musa Muhammed, pia aliumia katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Madagascar, na kwa sababu hiyo atakosa mchezo dhidi ya DR Congo lakini atakuwa tayari kwa ajili ya AFCON.

Advertisement

“Musa pia aliumia kwenye mchezo wetu na Madagascar, hatuwezi kumtumia dhidi ya DR Congo, kwani hiyo ni hatari kwetu, lakini niwahakikishie tu kuwa tuko vizuri na Musa atarejea kwa ajili ya AFCON," alisema.

MBADALA

Kukosekana kwa Mandela, kunamaanisha kuwa, Stars itamgeukia beki wa Gor Mahia, Joash Onyango kwa mujibu wa Migne, kikosi chake kimetimia zaidi kukabiliana na matatizo kama hayo kama ilivyokuwa kwenye mchezo wa kufuzu dhidi ya Ghana.

“Tuliwafunga Ghana bila ya uwepo wa maproo wetu, tunaamini tunaenda kufanya hivyo dhidi ya Congo na timu yoyote ile bila woga. Joash pamoja na wachezaji wengine wazoezi wapo tayari kuziba haya mapengo," alisema Migne.

Baada ya mechi ya DR Congo, Stars itaelekea Cairo (Juni 19), kwa ajili ya AFCON zitakazoanza Juni 21 hadi 19. Kenya ambayo iko katika kundi C, itatupa karata yake ya kwanza Juni 23 dhidi ya Algeria, kisha itacheza na Tanzania (Juni 27) kabla ya kuwavaa Senegal, Julai mosi. Mechi zote zitapigwa katika uwanja wa Cairo June 30.

 

 

Advertisement