Werner awaaga kibabe RB Leipzig

Monday June 29 2020
werner pic

Munich, Ujerumani. MASHABIKI wa Chelsea utawaambia nini kuhusu straika wao mpya Timo Werner, ambaye juzi usiku alicheza mechi yake ya mwisho akiwa na RB Leipzig na kutupia mabao mawili kwenye ushindi wa 2-1 dhidi ya Augsburg.

Mchezo huo ulikuwa wa mwisho kwa Werner na kuhitimisha Ligi Kuu Ujerumani maarufu Bundesliga, ambapo kama kawaida Bayern Munich walishatangaza ubingwa muda mrefu tu.

Werner, 24, kwa sasa ni mchezaji wa Chelsea baada ya kusaini mkataba wa miaka mitano na alishatambulishwa kwenye tovuti na mitandao ya kijamii ya wababe hao wa Jiji la London.

Mabao hayo mawili yamemfanya Werner kuifungia RB Leipzig mabao 28 msimu huu na hilo, limezidi kuwapa mzuka mashabiki wa Chelsea. Werner anatarajiwa kujiunga na wachezaji wenzake mwezi ujao tayari kwa kujipanga kwa msimu mpya wa Ligi Kuu England.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Werner alisema: “Najisikia mwenye furaha kwa kuwaaga mashabiki wangu kwa mabao na ushindi pia. Ni furaha zaidi kuona nimekuwa mfungaji bora wa muda wote wa RB na hilo litabaki ndani ya moyo wangu. Nitawakumiss sana mashabiki, wachezaji na viongozi.”

Advertisement