Straika Simba ataja kipa mpya

Mshambuliaji nyota wa zamani wa klabu ya Simba, Zamoyoni Mogella.
Mshambuliaji nyota wa zamani wa klabu ya Simba, Zamoyoni Mogella amekiangalia kikosi cha timu hiyo kipindi hiki kuelekea kwenye usajili wa dirisha kubwa na kueleza kuwa inahitaji maboresho maeneo yote.
Mogella amekwenda mbali zaidi na kueleza kuwa kikosi hicho kinahitaji kusajili kipya mpya mwenye ubora stahiki au kuwatumia vizuri waliopo ikiwa ni pamoja na kumpa nafasi Beno Kakolanya ambaye muda mwingi amekuwa akikalishwa benchi na Aishi Manula.
“Simba inajaribu kuwa ya kimataifa, lakini bado usajili wake hauendani na nyota wanaoweza kutoa ushindani wa kimataifa,” alisema Mogella ambaye aliwahi kupachikwa jina la Golden Boy kwa umahiri wake wa kuzifumania nyavu.
Alisema Simba ikifikia uwezo wa kusajili mchezaji wa kima cha chini kwa Sh700 milioni ndipo itaingia anga za kimataifa na hata kutwaa ubingwa wa Afrika, lakini kwa sasa levo yao bado ni ya ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Ukanda wa Cecafa.
Akizungumzia usajili wa dirisha kubwa msimu huu, Mogella alisema kikosi hicho kinatakiwa kuboreshwa kuanzia kwenye nafasi ya kipa hadi ushambuliaji.
“Kwenye ushambuliaji binafsi naona anayestahili kubaki ni Kagere, wengine bado, lakini kwa kuwa wanashindana katika ligi yetu tunaona ni sawa,” alisema.
Alisema kwenye makipa bado kuna udhaifu, huenda kuna matumizi mabovu juu ya waliopo, hivyo kunahitajika kipa ambaye ataongeza ushindani wa namba katika kikosi hicho.
“Mabeki nako kuna udhaifu mkubwa, hili eneo ndiko kunahitaji kuboreshwa hasa katika kikosi cha Simba, kifupi kila idara kwenye kikosi cha Simba kunahitaji kuboreshwa wakati huu na si kwa Simba tu hata Yanga na timu zingine.
“Huwezi kuwa na mshambuliaji wa kimataifa msimu mzima hata goli 10 hafikishi unabaki naye, wa nini? au mchezaji msimu mzima anapangwa mechi tatu tena akitokea benchi,” alisema Mogella.