Makame afunguka bao la kujifunga Yanga

Dar es Salaam. Kiungo wa Yanga, Abdulaziz Makame ameomba radhi mashabiki wa klabu hiyo, baada ya juzi kujifunga katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zesco United ya Zambia.

Mchezaji huyo alisema tukio hilo ni baya zaidi kutokea kwake tangu alipoanza kucheza soka.

Akizungumza jana, Makame amewataka mashabiki kusahau bao hilo na kujiandaa vyema kwa mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Makame aliyecheza kwa kiwango bora katika mechi zote mbili za nyumbani na ugenini, alijifunga bao dakika ya 78 katika harakati ya kuokoa kiki ya mpira wa krosi iliyopigwa upande wa kushoto na winga Quadri Aladeokun.

Akizungumzia bao hilo, Makame alisema lengo lake lilikuwa kutoa mpira nje baada ya kuona anakabiliwa na wachezaji wawili wa Zesco nyuma yake.

“Nilikwenda kasi kuzuia mpira baada ya kuona nyuma yangu kuna wachezaji wa Zesco, nikiwa na uhakika wa kutoa nje bahati mbaya nikajifunga,”alisema Makame.

Kiungo huyo aliyejiunga na Yanga akitokea Mafunzo ya Zanzibar, alisema kilichotokea ni sehemu ya mchezo na amewataka wadau wa klabu hiyo kujipanga kwa Kombe la Shirikisho.

Makame alisema Yanga inapaswa kufanya maandalizi ya kutosha kwa kuwa mashindano hayo yanashirikisha timu zenye uzoefu, hivyo wanapaswa kujiandaa kikamilifu.

Kiungo huyo alikuwa nyota wa mchezo wa kwanza kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam waliotoka sare ya bao 1-1.

Baada ya mchezo huo, Kocha wa Zesco, George Lwandamina alisema Makame ni mchezaji wa aina yake na alikuwa kikwazo kwa timu yake kupata ushindi.

Lwandamina alisema tukio la kujifunga linaweza kumpata mchezaji yeyote na sehemu ya mpira.

“Ni tukio la bahati mbaya yule kijana ni hodari sana katika nafasi ya kiungo.

Jambo hili lingeweza pia kumpata mchezaji wangu. Lakini wenye nafasi ya kumjenga au kumbomoa ni wachezaji wenzake na benchi la ufundi la Yanga kwa namna watakavyopokea tukio lile,” alisema Lwandamina.

Timu nyingine zilizoungana na Yanga kucheza Kombe la Shirikisho zikitokea Ligi ya Mabingwa Afrika ni KCCA (Uganda), UD Songo (Msumbiji), Elect-Sport (Chad), Cano Sport (Equatorial Guinea), Al-Nasr (Libya) na Côte d’Or (Shelisheli).