JICHO LA MWEWE: Dola milioni moja kwa Prince Dube haikataliki kamwe

WAZIMBABWE walituletea habari majuzi kwamba mshambuliaji wao, Prince Dube anatakiwa na klabu ya Raja Casablanca ya Morocco. Mchezaji Mzimbabwe anacheza Tanzania, anatakiwa Morocco lakini habari zinatoka kwao Zimbabwe. Dunia ya sasa!

Azam wamedai hawana ofa ya dola milioni moja (Shilingi 2.3 bilioni) mezani kutoka kwa Wamorocco. Huenda ni uvumi wa kawaida au huenda kuna ukweli. Kama unataka kuhisi kuna ukweli unaweza kutumia mambo mawili kukisia kwamba ni habari ya kweli.

Kwanza kabisa wachezaji wa Zimbabwe wanauzika kila pembe ya dunia. Wenzetu sio kama sisi. Hata mchezaji wa kwanza Mwafrika kucheza Ligi Kuu ya England katika mfumo mpya alikuwa Mzimbabwe. Peter Ndlovu. Kwahiyo haishangazi sana. Wanaujua mpira. Pale Afrika Kusini wametawala kwa kiasi kikubwa.

Lakini msingi mwingine ni ukweli kwamba Wamorocco wana uwezo wa kutoa kiasi cha pesa kilichotajwa. Dola milioni moja. Wamewahi kulipa kiasi kikubwa zaidi ya hiki. Unapounganisha hisia hizi mbili unagundua kwamba kuna uwezekano habari kama hii ikawa kweli.

Iwe kweli au sio kweli lakini nilishangazwa kidogo na majibu kutoka kwa baadhi ya watendaji. Mtendaji mkuu rafiki yangu, Abdulkarim Popat alidai kwamba hata kama ni kweli dili hilo lipo bado hawana mpango wa kumuuza Dube kwenda kokote kule. Nilishangazwa kidogo.

Msemaji wao, Zaka Zakazi naye alikuwa na mtazamo huo huo. Nilishangazwa zaidi. Hata hivyo, kitu cha muhimu kingekuwa kujua matajiri wa timu, familia ya Bakhresa, wangekuwa na msimamo gani kama ofa ingekuwa mezani.

Ukweli ni kwamba ofa kama hiyo haikataliki. Dube wamemchukua kwa shilingi ngapi kutoka alikokuwa? Tuseme ameigharimu Azam dola 200,000. Bado ni faida kwao kama wakimuuza dola milioni moja. Huu ni mfano tu, siamini kama Azam wametumia kiasi cha dola 200,000 kumpata Dube. Faida ya namna hii haikataliki.

Lakini nilimsikia pia rafiki yangu Popat akidai kwamba lengo lao kubwa ni kutwaa ubingwa msimu huu lakini pia kuisaka michuano ya kimataifa. Unajiuliza. Wakitwaa ubingwa watapata kiasi gani? Tufanye shilingi 100 milioni. Kumbuka kwamba bei ya Dube ni shilingi 2.3 bilioni. Unakataaje kwa sababu ya shilingi 100 milioni? Swali ambalo jibu lake ni rahisi.

Hapo hapo unajiuliza. Azam wana mpango upi msimu huu na ujao. Kwamba watachukua ubingwa? Sawa. Kwamba baada ya hapo wataenda michuano ya Afrika na kuchukua ubingwa? Bado zawadi ya ubingwa haiwezi kuwa sawa na mauzo ya Dube. Kwanini asiuzwe? Lakini vile hayo yote mawili ni bahati nasibu. Unaweza kuwa na Dube na usitwae na ubingwa wa Tanzania. Lakini hapo hapo tunajiuliza swali jingine la msingi. Azam wamewekeza vya kutosha katika kikosi chao kiasi cha kukataa ofa ya Dube?

Hapa nina maana hii. Hizi klabu kubwa za Afrika Kaskazini kama Al Ahly, Raja, Wydad, Zamalek na nyinginezo zimefanya uwekezaji katika maeneo mengi uwanjani kiasi kwamba mchezaji kama Dube akiwa katika kikosi chao anakuwa mmoja kati ya mastaa ambao wanakamilisha kikosi kizuri.

Dube ni mwanzo wa uwekezaji mkubwa wa Azam? Sidhani hivyo. Kando yake kuna wachezaji wengi wa kawaida ambao hawawezi kupambania ubingwa wa Afrika. Hao wenzetu wana wachezaji wengi wanaoweza kuipambania timu kuchukua ubingwa wa Afrika kiasi kwamba wanaweza kumzuia mchezaji mmoja asiondoke.

Hii ni hadithi ya kina Ajax Amsterdam au Borussia Dortmund. Hawawezi kumbakisha mchezaji kwa ajili ya kuwania mataji. Wanajua hawapo katika viwango hivyo. Wanachohakikisha wanafanya ni kuuza mastaa wakubwa zaidi kwa sababu ya kibiashara. Staa mkubwa zaidi anayechomoza anawekwa sokoni.

Ukiachana na hilo, binafsi nilikuwa natamani dili kama hili litokee ili liamshe Watanzania. Pesa ya soka ni tamu. Kama lingetokea nadhani klabu zetu zingeanza kufungua milango ya biashara hii ya mauzo ya wachezaji.

Kuanzia hapo wangeanza hata kuwekeza kwa wachezaji vijana zaidi ndani na nje ya nchi. Iko wazi kwamba wachezaji wengi wa kigeni wanaotamba nchini umri umewatupa mkono na ni ngumu kwao kuuzika. Huyu Dube anaingia katika tetesi kwa sababu umri wake unasadifu biashara. Miaka 23 tu.

Pesa ya mauzo ya wachezaji huwa inatatua matatizo mengi klabuni. Jaribu kufikiria kama Dube angekuwa mchezaji wa Yanga halafu dili kama hilo likaja mezani. Wangekuwa na uwezo wa kujenga viwanja vizuri vya mazoezi katika eneo lao la Kigamboni walilopewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam aliyepita, Paul Makonda.

Nakumbuka walichofanya Arsenal baada ya kumuuza mshambuliaji wao mtukutu, Nicolas Anelka kwa dau la Pauni 22 milioni kwenda Real Madrid mwaka 1999. Kilikuwa kiasi kikubwa cha pesa ambacho kiliwawezesha kufanya mambo mawili.

Kwanza walitumia kiasi cha Pauni 10 milioni kujenga uwanja wao mpya wa mazoezi London Colney lakini pia walitumia kiasi kilichobaki kumnunua Thierry Henry kutoka Juventus. Henry akafanya mambo makubwa zaidi.