BEBABEBA: Madrid yaanza na Mane kisha Mbappe

MADRID HISPANIA. NI suala la kuchagua, Sadio Mane au Kylian Mbappe. Hicho ndicho inachopanga kukifanya Real Madrid kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi kwamba, nani aanze kutua Bernabeu.

Kocha, Zinedine Zidane anahitaji kuongeza makali kwenye safu yake ya ushambuliaji katika chama lake la Los Blancos ili kuwa moto zaidi msimu ujao na sasa mezani kuna majina mawili ya kuanza nayo wakati dirisha la majira ya kiangazi litakapofunguliwa.

Majina hayo ni Mane na Mbappe. Lakini, kwa mujibu wa ripoti zilizopatikana kutoka Hispania ni kwamba, Real Madrid imeamua kuwekeza nguvu yao kubwa kwenye kumnasa staa wa Liverpool, Mane na kuachana na Mbappe katika uhamisho wa mwaka huu.

Madrid wamegundua kwamba itakuwa ngumu kuwashawishi Paris Saint-Germain na kupata huduma ya Mbappe mwaka huu, huku wakiamini kwamba kwenye dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi la mwakani watampata mchezaji huyo kwa dau dogo zaidi.

PSG hawataki kabisa kuzungumza kuhusu kumuuza staa wao Mbappe kwenda Madrid mwaka huu na sasa Zidane amegeuza kibao kwa Mane, anayetajwa kuwa na thamani ya Pauni 131 milioni.

Na sasa Madrid wamepanga kumchukua Mane mwaka huu na mwakani watakamilisha dili la kunasa huduma ya Mbappe.

Mabosi wa Real Madrid wanachokiamini ni kwamba, ni wao tu ndio watakaomshawishi Mane kubeba virago vyake na kuachana na miamba hiyo ya Anfield.

France Football limeshatoa ripoti likidai kwamba Mane, 28, amekuwa hana furaha huko Anfield baada ya kocha Jurgen Klopp kutumia nguvu nyingi kupigania Virgil van Dijk abebe tuzo ya Ballon d’Or kuliko yeye.

Na sasa, Le10sport linaripoti kwamba Zidane anadhani hiyo ni fursa ya kumbeba Mane kwenye dirisha lijalo na Mbappe watamalizana naye kwenye majira ya kiangazi ya mwaka 2021.

Real Madrid inaripotiwa kwamba kwa mara ya kwanza ilifanya mawasiliano ya kumnasa Mane, Julai mwaka jana, walipojaribu kuona kama wangenasa saini yake baada ya kutoka kuwapa Liverpool ubingwa wa Ulaya. Na sasa mwaka mmoja umepita, Zidane anahitaji mrithi wa Karim Benzema, 32. Liverpool wanamtaka Mane abaki baada ya kuona amekuwa kwenye ubora mkubwa na kuziba pengo Mo Salah asipokuwepo au akicheza chini ya kiwango.

Lakini, Klopp kwa sasa yupo bize kusaka saini ya fowadi wa RB Leipzig, Timo Werner, ambaye kwa mujibu wa kipengele kilichowekwa kwenye mkataba wake, timu yoyote inaweza kumnasa kwa Pauni 52 milioni tu. Fowadi huyo Mjerumani, Werner mwenyewe alisema wazi kwamba ni heri kuhamia ng’ambo kuliko kwenda kujiunga na Bayern Munich ambao, ndi wababe wa Bundesliga.

Liverpool ndiyo inayopewa nafasi kubwa ya kunasa saini yake, licha ya ripoti nyingine kudai kwamba Chelsea nao wameonyesha dhamira ya dhati ya kunasa huduma ya mshambuliaji huyo matata kabisa kwenye Bundesliga mwishoni mwa msimu huu.