Simulizi ya Antony alivyoishi siku 40 za mateso Man United
Muktasari:
- Antony, ambaye alisajiliwa na Man United Agosti 30, 2022, kwa dau kubwa la pauni milioni 86 akitokea Ajax, aliishia kuwa moja ya usajili mbovu baada ya klabu hiyo kupata hasara ya karibu pauni milioni 60 katika mauzo yake dakika za lala salama ya dirisha la usajili lililopita.
MANCHESTER, ENGLAND: WINGA wa zamani wa Manchester United, Antony, ametoa malalamiko kuhusu namna alivyotendewa vibaya wakati akiwa sehemu ya wachezaji waliotengwa ndani ya kikosi hicho chini ya kocha Ruben Amorim, kabla ya msimu huu kuondoka rasmi na kutua Real Betis.
Antony, ambaye alisajiliwa na Man United Agosti 30, 2022, kwa dau kubwa la pauni milioni 86 akitokea Ajax, aliishia kuwa moja ya usajili mbovu baada ya klabu hiyo kupata hasara ya karibu pauni milioni 60 katika mauzo yake dakika za lala salama ya dirisha la usajili lililopita.
Awali maisha yake ndani ya Man United yalikuwa mazuri akifanikiwa kusaidia kushinda mataji mawili, Carabao mwaka 2023 na Kombe la FA 2024. Baada ya hapo, mambo yakageuka.
Nyota huyo raia wa Brazil, ameeleza kuwa aliishi maisha magumu akiwa ameachwa nje ya kikosi cha kwanza, ambapo alitumia zaidi ya siku 40 akiishi katika hoteli ya uwanja wa ndege jijini Manchester, akilipa pauni 175 kwa usiku, huku akifanya mazoezi kivyake.
Akizungumza na El Desmarque, Antony amesema: “Ilikuwa miezi migumu sana nchini England, zaidi ya siku 40 hotelini, kufanya mazoezi peke yangu… Nahisi nilidharauliwa, lakini sitaki kuanzisha malumbano. Hayo ni maisha. Nashukuru kwa klabu, kulikuwa na nyakati mbaya na pia nzuri, tulipata mataji mawili.”
Antony ameweka wazi kuwa familia yake ilitangulia kuhamia Mji wa Seville siku chache kabla ya dili la kurejea Betis kukamilika, tayari akiwa ameshapangisha nyumba.
Hoteli aliyofikia, Delta Hotels Manchester Airport Marriott, ina wastani wa alama 3.6/5 kwenye TripAdvisor, huku baadhi ya wageni wakilalamikia vyumba vibovu, usafi hafifu na hata kuonekana kwa mende.
Hii ilikuwa hitimisho la aibu kwa muda wake United, ambapo alicheza mechi 96 na kufunga mabao 12 pekee ndani ya misimu mitatu. Katika nusu msimu uliopita alifunga bao moja pekee kwenye michezo 14 kabla ya kupelekwa kwa mkopo Betis, ambako alifanya vizuri kwa kufunga mabao tisa na asisti tano kwenye mechi 26, na sasa amesajiliwa moja kwa moja kikosini hapo.
Wakati wa utambulisho wake huko Hispania, Antony alishindwa kujizuia machozi akieleza: “Ni mimi pekee najua ugumu wa maisha yangu Manchester. Kufanya mazoezi peke yangu… lakini sasa yamepita. Sevilla ni nzuri zaidi kuliko Manchester, nafurahi kuwa hapa.”
Aliongeza: “Nilikaa zaidi ya siku 40 hotelini, ilikuwa ngumu sana, lakini kila mtu alijua nataka kurudi Betis. Niko nyumbani sasa, nina furaha katika mji na klabu ninayoipenda. Nikivaa jezi, nitapambana kwa ajili ya kila shabiki wa Betis.”
Msimu huu Antony bado hajafunga wala kutoa pasi ya bao kwenye michezo mitatu ya La Liga, ingawa amefunga dhidi ya Nottingham Forest kwenye Europa League wakati matokeo yakiwa 2-2 ambapo pia alitoa asisti.
Ikumbukwe kuwa, baada ya mambo kuwa magumu ndani ya Man United, Januari 25, 2025, alipelekwa Real Betis kwa mkopo kabla ya hivi karibuni kusajiliwa moja kwa moja.