Sikia hii ya Xavi Simons
Muktasari:
- Simons, 22, anasakwa kwa nguvu zote na The Blues na ameshafikia makubaliano ya mdomo huku dili hilo likidaiwa kuwa kwenye hatua za mwisho.
LONDON, ENGLAND: STAA anayesakwa na Chelsea, Xavi Simons amefuta maneno yote yanayotaja RB Leipzig kwenye wasifu wake wa kurasa zake za mtandaoni.
Simons, 22, anasakwa kwa nguvu zote na The Blues na ameshafikia makubaliano ya mdomo huku dili hilo likidaiwa kuwa kwenye hatua za mwisho.
Klabu yake ya Ujerumani inataka ada ya Pauni 60 milioni na Chelsea ipo tayari kupeleka ofa yake ya kwanza rasmi.
Na katika kuchochea uvumi huo, kiungo huyo mshambuliaji Simons amefuta maelezo ya kwamba ni mchezaji wa RB Leipzig kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii.
Kitu pekee alichokiacha kwenye ukurasa huo ni maelezo ya kwamba yeye ni balozi wa hisani wa Unicef na pia amekuwa akidhaminiwa na Puma. Lakini, posti yake akiwa amevaa jezi ya RB Leipzig hajazifuta.
Na mashabiki wa mtandaoni wamedaiwa kwa siku za hivi karibuni walimwona staa huyo akiwawafolo mastaa wa Chelsea kama Liam Delap, Levi Colwill na Romeo Lavia kwenye kurasa zao za mtandao wa Instagram.
Mashabiki wanaamini Chelsea itafanikiwa kunasa saini ya kiungo huyo wa ushambuliaji na kumvuta Stamford Bridge kabla ya dirisha hili kufungwa.
Shabiki wa kwanza alisema: “Hii kitu inakwenda kutokea.”
Mwingine aliongeza: “Hii hapa, imethibitika.”
Shabiki wa tatu alisema: “Kinachoonekana ni kama makubaliano binafsi yameshafikiwa.”
Kwenye dili hilo, Chelsea imewaorodhesha mastaa Christopher Nkunku, Armando Broja, Tyrique George na Carney Chukwuemeka kuwa sehemu ya dili kwa kubadilishana na klabu hiyo ya Ujerumani, lakini yenyewe imeng’ang’ania kutaka Pauni 60 milioni.