Shughuli imeisha, mwamba karudi nyumbani
Muktasari:
- Mourinho (62), ambaye ni mshindi mara mbili wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, amesaini mkataba wa miaka miwili utakaoisha mwishoni mwa msimu wa 2026/27. Hii inakuja baada ya kufutwa kazi na Fenerbahce mwezi uliopita kufuatia kushindwa kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kocha mkongwe Jose Mourinho amerudi tena nyumbani, baada ya kutangazwa rasmi kuwa kocha mpya wa Benfica, klabu kubwa ya Ureno ambayo aliwahi kuinoa kwa muda mfupi mwaka 2000.
Mourinho (62), ambaye ni mshindi mara mbili wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, amesaini mkataba wa miaka miwili utakaoisha mwishoni mwa msimu wa 2026/27. Hii inakuja baada ya kufutwa kazi na Fenerbahce mwezi uliopita kufuatia kushindwa kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Akizungumza kwenye utambulisho wake, Mourinho hakusita kuzungumzia safari yake akisema:
“Nilikosea kwenda Fenerbahce, lakini sikujutia. Nilitoa kila kitu hadi siku ya mwisho. Kuinoa Benfica ni kurudi kwenye kiwango changu.”
Mourinho ameahidi kuirudisha Benfica kileleni, akisisitiza kikosi hicho kina kila kitu cha kushinda Ubingwa msimu huu licha ya kuanza kwa mtikisiko.
Rais wa klabu, Rui Costa, amesema:
“Mourinho hahitaji utambulisho. Ni fahari na heshima kubwa kumpata tena hapa Benfica. Tunataka kocha mwenye rekodi ya ushindi na ni vigumu kumpata mtu aliye na historia ndefu kuliko yeye.”
Mourinho alianza kazi yake Benfica mwaka 2000 kabla ya kuondoka baada ya mechi 10 tu, na baadaye kupata mafanikio makubwa akishinda makombe makubwa akiwa na Porto, Chelsea, Inter Milan, Real Madrid, Manchester United na Roma.
Kurudi kwake sasa kunakoleza hamasa hasa ikizingatiwa kwamba mwezi huu Benfica watakutana na Chelsea katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, klabu ambayo Mourinho aliwahi kushinda nayo mataji matatu ya Ligi Kuu England.
Kwa sasa Benfica ipo nafasi ya sita kwenye Ligi ya Ureno ikiwa pointi tano nyuma ya vinara Porto, na Mourinho anatarajiwa kuanza rasmi majukumu yake wikiendi hii dhidi ya Vila das Aves timu ambayo nayo aliwahi kuinoa kipindi cha nyuma.