Ronaldo amtaka Casemiro fasta Al Nassr
Muktasari:
- Kiungo wa Kibrazili, Casemiro, ambaye alikuwa mchezaji mwenzake Ronaldo kwenye kikosi cha Real Madrid, ameonekana kukosa nafasi kwenye kikosi cha sasa cha Manchester United chini ya Kocha Ruben Amorim huko Old Trafford.
RIYADH, SAUDI ARABIA: SUPASTAA, Cristiano Ronaldo ametaka mabosi wa Al Nassr kufanya kweli kumvuta Casemiro kwenye Saudi Pro League mwezi huu.
Kiungo wa Kibrazili, Casemiro, ambaye alikuwa mchezaji mwenzake Ronaldo kwenye kikosi cha Real Madrid, ameonekana kukosa nafasi kwenye kikosi cha sasa cha Manchester United chini ya Kocha Ruben Amorim huko Old Trafford.
Licha ya Casemiro kupungua makali yake msimu huu, Ronaldo anaamini bado ni mmoja wa viungo matata kabisa wa Ulaya wanaopaswa kwenda kubandisha hadhi ya soka la Saudia.
Kwa mujibu wa Daily Star, Man United inakaribisha ofa za kumhusu kiungo Casemiro, ambaye mshahara wake wa zaidi ya Pauni 300,000 anaolipwa kwa wiki unaonekana kuwa mzigo kwa sasa kwenye bili ya mishahara ya klabu hiyo ya Old Trafford.
Casemiro, 32, hajaichezea Man United tangu ilipokutana na kichapo kutoka kwa Newcastle United mwishoni mwa Desemba mwaka jana na kwa sasa kocha Amorim amekuwa akiwapa nafasi Manuel Ugarte na kiungo Bruno Fernandes kwenye eneo la kiungo la timu hiyo.
Kiungo kinda Toby Collyer naye amekuwa akipewa nafasi ya kuonyesha kipaji chake sambamba na Kobbie Mainoo na hivyo kumfanya Casemiro awe benchi.
Baada ya Casemiro kuwekwa benchi kwenye mechi Europa League dhidi ya Rangers, Alhamisi iliyopita, Amorim aliulizwa kama Mbrazili huyo yupo fiti kucheza kwenye mtindo wake wa fomesheni ya 3-4-2-1, ambapo Mreno huyo alisema:
“Anapaswa kuwa na vigezo tunavyotaka kwa sababu tunachagua mchezaji kwa vigezo vilivyopo kwa kuzingatia mechi.”