Pep aunda tume kuisambaratisha Manchester United kwao
Muktasari:
Kwenye baadhi ya magazeti ilidaiwa uamuzi anaoufanya Pep wa kuidharau Bundesliga kwa sababu tu tayari ana taji mkononi, kocha huyo atakuwa anahatarisha uwezekano wa timu hiyo kutwaa mataji matatu ingawa Pep mwenyewe hakuonekana kusumbuliwa na shutuma hizo.
TOLEO lililopita kwenye kitabu cha Pep Confidential, tuliona jinsi Mwandishi Marti Perarnau alivyolichambua tukio la Kocha Pep Guardiola kudharau mechi za Bundesliga na lawama alizokuwa akitupiwa kwenye vyombo vya habari na wachambuzi mbalimbali kwa hatua yake hiyo. Sasa endelea…
Kwenye baadhi ya magazeti ilidaiwa uamuzi anaoufanya Pep wa kuidharau Bundesliga kwa sababu tu tayari ana taji mkononi, kocha huyo atakuwa anahatarisha uwezekano wa timu hiyo kutwaa mataji matatu ingawa Pep mwenyewe hakuonekana kusumbuliwa na shutuma hizo.
“Kukosolewa baada ya kufanya jambo ni kitu chenye manufaa, kwa hali ilivyo ni jambo la msingi kwa klabu kubwa kama hii yetu, nikiri baadhi ya watu wanadhani inaniumiza mimi lakini kwa hakika hakuna kitu hicho.
Ukosoaji maana yake ni kukufanya uwe makini, ndiyo maana huwa napenda kujikosoa mwenyewe pamoja na wachezaji wangu.
Pep aliwaacha wachezaji wake watatu muhimu Lahm, Ribery na Robben katika mechi ya nyumbani dhidi ya Agsburg iliyochezwa Jumamosi na kuwaruhusu wachezaji wote kupumzika Jumapili. Alitaka wachezaji wapumzike ili wawe freshi kwa mazoezi ya asubuhi na jioni Jumatatu.
Alitaka kuwa na muda wa kupitia mipango yake kwa wachezaji wake na kuwataka wawe makini kadiri iwezekanavyo, hii haitokuwa mipango ya kawaida ya mechi.
Pep na wasaidizi wake, Torrent, Planchart na wachambuzi wengine waliifanyia tathmin Manchester United kwa mapana huku wakichambua kila eneo, walifanya uchambuzi kwa mapana kuhusu wapinzani wao ambao hadi saa tatu ya Jumatatu walikuwa wamekubaliana mpango wa mchezo huo utakavyokuwa pamoja na kikosi cha kwanza.
Pep aliutumia muda wa asubuhi ile na mchana kushirikisha mpango wake ule na watu wake wengine wa karibu, kwanza walifanyia kazi namna ambavyo timu hiyo ya England inavyocheza katika kushambulia na kukaba na namna wanavyoitumia mipira iliyokufa.
Waliyaangalia yote hayo kupitia mikanda ya video na baadaye kuifanyia kazi wakiwa mazoezini na wachezaji, Pep kwa mara nyingine alisisitiza jambo moja, kwenye mechi ya Old Trafford Man United walisababisha madhara makubwa mawili, mtu na mtu kati ya Welbeck na Neuer na bao la Vidic.
Malengo ya Bayern yaliweka mkazo katika maandalizi ya mechi hii, umakini katika kutumia mipira wanayoimiliki na kutoa nafasi chache mno nyumbani kuliko ilivyokuwa ugenini Manchester.
Hadi Jumatatu asubuhi wachezaji nao tayari walikuwa na mawazo mazuri tu kuhusu kikosi cha kwanza, Javi Martinez na Schweinsteiger walikuwa na adhabu na Thiago alikuwa majeruhi (Thiago alikwenda Barcelona kwa ajili ya matibabu ya goti kwa Dk Cugat).
Kilichowashangaza wachezaji na kuwaacha midomo wazi ni mpango mzima wa mechi walioambiwa na Pep Jumanne mara baada ya chakula cha mchana, “Tutakwenda kutumia mfumo wa 2-3-3-2.”
Wachezaji walikuwa katika furaha, baada ya hapo Pep alianza kuitaja timu ambayo ilikuwa na Neuer, Boateng, Dante, Lahm, Kroos, Alaba, Robben, Gotze, Ribery, Muller na Mandzukic.
Si tu aliwatajia kikosi cha kwanza mapema kuliko muda wa kawiada uliozoeleka, lakini pia aliwaonyesha namna nyingine tofauti ya nne za kushambulia katika maeneo mbalimbali.
Alilizingatia hilo kutokana na ukweli katika mechi hiyo Bayern ilikuwa imejiandaa kushambulia kwa asilimia 75 ya mechi nzima na kukaa eneo la nusu ya uwanja upande wa wapinzani wao. Pep alitaka kuona eneo la ulinzi linajazwa na watu wawili na mabeki wawili wa pembeni wenye kupanda na kuwa karibu na Kroos.
Alishazungumza na Lahm na kumwambia kwa mapana anachotaka, na ingawa katika kikosi alikuwa amepangwa kama beki wa pembeni lakini hicho si kitu ambacho Pep alikihitaji kutoka kwa nahodha huyo.
Badala yake alitakiwa acheze kama kiungo katika mstari wenye wachezaji watatu, wengine ni Kroos na Alaba.
Zaidi ya hilo, kwa kuwa Kroos huwa anapenda kucheza kwa kuelekea kushoto zaidi, Lahm atatakiwa kuingia na kutawala eneo la kati na hivyo kuwafanya wacheze kama viungo wa kati wenye kupokea mipira kwa mabeki.
Itaendelea Jumanne ijayo.