Partey mahakamani wiki ijayo
Muktasari:
- Mchezaji huyo wa zamani wa Arsenal anapaswa kufika mahakama ya Old Bailey, London Jumatatu, Septemba 15 na awali alitarajiwa kuonekana mahakamani Jumanne ya Agosti 26.
LONDON, ENGLAND: KIUNGO wa Villlarreal na timu ya taifa ya Ghana, Thomas Partey anatakiwa kufika mahakamani kwa mashtaka ya ubakaji Septemba 15, siku moja kabla ya mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Tottenham, kwenye Uwanja wa Tottenham Hotspur.
Mchezaji huyo wa zamani wa Arsenal anapaswa kufika mahakama ya Old Bailey, London Jumatatu, Septemba 15 na awali alitarajiwa kuonekana mahakamani Jumanne ya Agosti 26.
Partey ameshtakiwa kwa makosa matano ya unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake wawili na alipewa dhamana mwanzoni mwa Agosti baada ya kusomewa mashtaka yake katika Mahakama ya Westminster Magistrates na kuyakana.
Kiungo huyu aliruhusiwa kuhamia Hispania na kujiunga na Villarreal chini ya masharti ya dhamana yake baada ya kuondoka Arsenal dirisha lililopita la majira ya kiangazi.
Uhamisho huo umepingwa sana na kikundi cha mashabiki wa Villarreal, pia alikashifiwa na baadhi ya mashabiki katika mchezo wa dabi dhidi ya Real Oviedo alipokuwa uwanjani.
Partey alishtakiwa na polisi siku nne baada ya kuondoka Arsenal na mechi ya Villarreal dhidi ya Tottenham, itakuwa ya kwanza kucheza katika ardhi ya England tangu aliposhtakiwa.
Kwa sasa Partey yuko katika majukumu ya kimataifa na timu ya taifa ya Ghana ambayo inacheza mechi za kufuzu Kombe la Dunia na jana iliumana na Chad.