Paqueta msafi ishu ya kubeti
Muktasari:
- Staa huyo wa West Ham United na Brazil kwa miaka miwili amekuwa akicheza huku akikabiliwa na tuhuma za kuhusika kwenye kubeti.
LONDON, ENGLAND: KIUNGO wa boli, Lucas Paqueta anatarajiwa kusafishwa kwenye sakata la tuhuma za kubeti zilizokuwa zikimkabili, imeripotiwa.
Staa huyo wa West Ham United na Brazil kwa miaka miwili amekuwa akicheza huku akikabiliwa na tuhuma za kuhusika kwenye kubeti.
Ni katika kilichokuwa kikidaiwa kwamba Paqueta alionyeshwa kadi za njano kwenye matukio manne tofauti kati na Novemba 2022 hadi Agosti 2023 na kwamba kadi hizo zilikuwa za kupanga. Hukumu ya tuhuma hizo endapo kama angekutwa na hatia, basi kiungo huyo angefungiwa maisha kujihusisha na soka.
Lakini, ripoti zinafichua Paqueta atasafishwa hakutenda kosa lolote na hilo litawekwa bayana wiki ijayo. West Ham na Paqueta waliripotiwa kuchukizwa na suala hilo kuchukua muda mrefu.
Na sasa FA italazimika kulipia gharama za kesi za kiungo huyo zinazokaribia Pauni 1 milioni. Muda mfupi kabla ya uchunguzi huo kuwekwa wazi, Manchester City ilikuwa imekubali kulipa Pauni 85 milioni kunasa huduma ya staa huyo wa zamani wa Lyon kutoka West Ham.
Lakini, dili hilo lilivunjika baada ya Man City kusikia ishu inayomkabili Paqueta.
Uchunguzi ulifanyika juu ya tuhuma hizo za kubeti kwamba zilianzia huko Brazil, mahali ambako staa huyo alizaliwa. Na kilichoelezwa beti ilikuwa ni kuanzia Pauni 7 hadi Pauni 400 ziliwekwa kwenye matukio manne tofauti ya kadi za njano alizoonyeshwa kiungo huyo kwenye mechi dhidi ya Leicester, Aston Villa, Leeds United na Bournemouth. Na kwamba jumla ya Pauni 100,000 zililipwa kwa mshindi kutokana na kadi hizo nne za njano.