Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Orlando yamaliza utawala wa miaka nane ya Mamelodi

Muktasari:

  • Hii ni taji la tatu kwa Pirates msimu huu katika kampeni ambayo itaendelea kukumbukwa kwa muda mrefu.

MASHABIKI wa Orlando Pirates hatimaye wameondoa kiu yao ya muda mrefu baada ya timu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini kufuatia ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Orbit College katika mchezo wa mwisho wa msimu uliochezwa leo Jumamosi Mei 23, 2026.

Hii ni taji la tatu kwa Pirates msimu huu katika kampeni ambayo itaendelea kukumbukwa kwa muda mrefu.

Ushindi huo umeifanya Pirates kumaliza ukame wa miaka 14 bila ubingwa wa ligi, ikitwaa taji la 10 la ligi kuu huku ikivunja utawala wa Mamelodi Sundowns ambayo ilikuwa imechukua ubingwa mara nane mfululizo.

Pirates sasa inakuwa timu ya kwanza tofauti na Sundowns kushinda ligi hiyo tangu Bidvest Wits ilipotwaa ubingwa mwaka 2017.

Kwa namna ilivyocheza msimu huu, Pirates ilistahili ubingwa huo. Wakati Sundowns ikipoteza pointi nyingi kwa sare nane ilizopata msimu huu, Pirates ilitumia vizuri makosa hayo.

Ilimaliza msimu wakiwa na pointi 69, pointi moja mbele ya Sundowns, huku pia wakiwa timu iliyoshinda mechi nyingi zaidi (21), kufunga mabao mengi zaidi (58) na kuruhusu mabao machache zaidi (12).

Baada ya kumaliza katika nafasi ya pili kwa misimu mitatu mfululizo bila kuisogelea sana Sundowns, huu ni msimu wa kipekee kwa klabu hiyo ya Soweto pamoja na kocha wao Abdeslam Ouaddou.

Ikumbukwe kuwa, Pirates ilitwaa pia mataji ya MTN8 na Carling Knockout, hivyo kukamilisha treble kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2012.

Pirates ilipata bao lao la kwanza dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza baada ya kipa wa Orbit, Sabelo Nkomo, kushindwa kuokoa kona iliyopigwa huku akijaribu kuupiga mpira mbali chini ya presha ya Thalente Mbatha na kujifunga mwenyewe.

Dakika nne baada ya kuanza kipindi cha pili, mchezaji wa zamani wa Pirates, Ndumiso Ngiba ambaye sasa anakipiga Orbit College, alijaribu kuokoa mpira mbele ya mshambuliaji Yanela Mbuthuma lakini akausukuma golini kwao.

Kupoteza mchezo huo kumethibitisha kushuka daraja kwa Orbit College baada ya msimu mmoja pekee katika ligi kuu ya Afrika Kusini.

Magesi FC imenusurika kushuka daraja moja kwa moja baada ya kuifunga Richards Bay bao 1-0, matokeo yaliyoiwezesha kupanda kutoka mkiani mwa msimamo. Hata hivyo, sasa itacheza mechi za mtoano za kupigania kubaki ligi kuu dhidi ya Cape Town City na Milford FC.

Orbit imemaliza msimu ikiwa na pointi 24 sawa na Magesi, lakini tofauti ya mabao ya Orbit ilikuwa -26 dhidi ya -19 ya Magesi.

Kwa upande mwingine, Marumo Gallants imepata sare yao ya saba mfululizo dhidi ya Stellenbosch na kujinusuru kushuka daraja kwa kumaliza na pointi 25.

Gallants imebakia ligi kuu licha ya kushinda mechi mbili pekee kati ya 28 za mwisho. Kama isingeanza msimu kwa ushindi dhidi ya Richards Bay na Orlando Pirates, huenda ingekuwa kwenye hatari kubwa zaidi.

Chippa United nayo ilikuwa kwenye hatari kabla ya mchezo wa mwisho wa msimu, lakini iliifunga Kaizer Chiefs bao 1-0 ugenini na kuhakikisha inaendelea kubaki ligi kuu kwa msimu mwingine.