Ofa ya Liverpool yapigwa chini St James’ Park
Muktasari:
- Inaelezwa kwamba Liverpool ilipeleka ofa ya Pauni 110 milioni pamoja na kiasi kidogo cha bonasi kwa ajili ya kumchukua straika huyo anayetaka kuhama.
NEWCASTLE, ENGLAND: HABARI ndo hiyo. Newcastle United imekataa ofa ya kwanza ya Liverpool kwa ajili ya mshambuliaji wao Alexander Isak.
Inaelezwa kwamba Liverpool ilipeleka ofa ya Pauni 110 milioni pamoja na kiasi kidogo cha bonasi kwa ajili ya kumchukua straika huyo anayetaka kuhama.
Newcastle inataka mshambuliaji wao huyo staa kubaki kwenye kikosi chao na kupambana kumsainisha dili jipya.
Kwenye mkataba huo mpya kuna kipengele pia cha kumruhusu kuondoka wakati wa dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi la mwakani.
Lakini, Isak sasa amepanga kuachana na timu hiyo licha ya kuzungumza na mastaa wenzake kwenye kikosi hicho cha St James’ Park.
Isak, 25, hakuwepo kwenye ziara ya pre-season ya Newcastle huko Asia, huku klabu yake ikidai kwamba mshambuliaji huyo ana maumivu ya paja. Na badala yake, amekuwa akifanya mazoezi kwenye klabu yake ya zamani ya Real Sociedad kwenye viwanja vya Zubieta.
Newcastle imekuwa ikisisitiza kwamba Isak hauzwi, huku staa huyo akibakiza mkataba wa miaka mitatu kwenye kikosi hicho. Na katika kufanikisha hilo, Newcastle imetaja bei ya Isak kuwa ni Pauni 150 milioni, mkwanja ambao utakuwa parefu kwa Liverpool kulipa.
Kwenye dirisha hilihili la majira ya kiangazi, Liverpool imevunja rekodi ya uhamisho Uingereza, wakati ilipotoa Pauni 116.5 milioni kunasa saini ya kiungo wa Bayer Leverkusen, Florian Wirtz. Liverpool pia imemsajili kwa pesa nyingi straika Hugo Ekitike.