Mtego wa Waarabu kwa Vini Jr ni balaa
Muktasari:
- Supastaa huyo wa Real Madrid anaweza kuingia kwenye dili la kuvunja rekodi ya dunia la kunaswa kwa Pauni 250 milioni kwenye dirisha la kiangazi.
RIYADH, SAUDI ARABIA: KLABU za soka za Saudi Arabia zimepanga kutumia zaidi ya Pauni 1 bilioni kuhakikisha zinamnasa Vinicius Jr akakipiga huko, imeripotiwa.
Supastaa huyo wa Real Madrid anaweza kuingia kwenye dili la kuvunja rekodi ya dunia la kunaswa kwa Pauni 250 milioni kwenye dirisha la kiangazi.
Vinicius kwa sasa anaweka kibindoni Pauni 17milioni kwa mwaka kutokana na huduma anayotoa kwenye kikosi hicho cha mabingwa wa La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya huko Bernabeu. Lakini, mabosi wa Saudi Arabia wanataka kumpa Pauni 168 milioni kwa mwaka. Ripoti kutoka Hispania zinadai Vinicius atapewa ofa ya mkataba wa miaka mitano, ambapo utakuwa na thamani ya Pauni 865 milioni.
Real Madrid dhamira yake ni kubaki na mchezaji huyo na kusisitiza kwamba ofa itakayoifanya kufikiria kumuuza itakaribia Pauni 1 bilioni kama ilivyoelezwa kwenye kipengele kilichowekwa katika mkataba kwa timu itakayotaka kuvunja.
Lakini, kinachoelezwa haitamzuia Vinicius asiondoke kama kutakuwa na ofa ya kutamanisha mezani. Staa huyo wa Kibrazili ameripotiwa kuwa na furaha kubwa Real Madrid, hivyo hajioni kabisa kama ataondoka licha ya kwamba Los Blancos italazimika kuboresha mshahara wake mwisho wa msimu.
Jambo hilo linawatisha Real Madrid kwamba licha ya kuwa na pesa za kutosha, lakini hawana uwezo wa kushindana na klabu za Saudi Arabia.
Klabu hizo za Saudi Arabia, mfano Al-Hilal, ambayo ilikuwa ikimlipa Neymar mshahara wa Pauni 2.5 milioni kwa wiki.