Mourinho amvulia kofia Pedro Neto
Muktasari:
- Leo Septemba 30, 2025, kikosi cha Mourinho kinatarajiwa kukabiliana na Chelsea katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku klabu zote mbili zikisaka pointi zao za kwanza kwenye michuano hiyo msimu huu.
Kocha wa Benfica, Jose Mourinho, amemsifu nyota wa Chelsea, Pedro Lomba Neto, kama mmoja wa wachezaji bora zaidi duniani kwa sasa, kufuatia kauli ya kiungo huyo kutamani kucheza chini ya uongozi wake.
Leo Septemba 30, 2025, kikosi cha Mourinho kinatarajiwa kukabiliana na Chelsea katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku klabu zote mbili zikisaka pointi zao za kwanza kwenye michuano hiyo msimu huu.
Pedro Neto, ambaye ni mchezaji wa kimataifa wa Ureno, alimsifu Mourinho kama mtu aliyebadilisha soka la Ureno huku akitamani kufundishwa na kocha huyo.
Kocha huyo wa zamani wa Real Madrid, ameonyesha heshima kwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 katika mkutano wake na waandishi wa habari, lakini alikiri kuwa Benfica haiwezi kumudu gharama za mchezaji wa hadhi kama Neto.
"Neto ni mmoja wa mawinga bora zaidi duniani. Enzo Maresca ana bahati kwa kuwa na wachezaji watatu au wanne wenye aina hiyo ya uchezaji. Bila shaka, ningependa kuwa na Pedro Neto Benfica, lakini anacheza katika mazingira tofauti yenye hali tofauti ya kifedha," amesema.
Maandalizi ya mechi kati ya Chelsea na Benfica yamezingirwa na tukio la kurejea kwa Jose Mourinho katika Uwanja wa Stamford Bridge. Kocha huyo alifurahia vipindi viwili vya mafanikio makubwa katika klabu hiyo ya London, akishinda taji la Ligi Kuu ya England mara tatu.
Mourinho ameteuliwa kuwa kocha wa Benfica baada ya klabu hiyo kuachana na Bruno Lage kufuatia kichapo kutoka kwa Qarabag katika mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya wiki mbili zilizopita. Mourinho, anayejulikana kama 'The Special One', alifutwa kazi na Fenerbahce mapema msimu huu baada ya kutolewa na Benfica katika hatua ya kufuzu Ligi ya Mabingwa.