Mo Salah: Ekitike? Bado hatujawezana
Muktasari:
- Salah anacheza kwenye safu mpya ya ushambuliaji ya Liverpool sambamba na Ekitike na Florian Wirtz, huku Alexander Isak akijiunga kwenda kuongeza nguvu kwenye safu hiyo.
LIVERPOOL, ENGLAND: SUPASTAA wa Liverpool, Mohamed Salah amekiri kwamba bado hajaelewana vyema na mshambuliaji mwenzake kwenye kikosi hicho, Hugo Ekitike.
Salah anacheza kwenye safu mpya ya ushambuliaji ya Liverpool sambamba na Ekitike na Florian Wirtz, huku Alexander Isak akijiunga kwenda kuongeza nguvu kwenye safu hiyo.
Liverpool imetumia Pauni 450 milioni kunasa mastaa wapya kwenye dirisha hili, huku ikitumia pesa nyingi sana kuwasajili Isak, Wirtz na Ekitike. Wakali hao wametua kwenda kuchukua nafasi za Luis Diaz na Darwin Nunez, walioondoka dirisha hili na Diogo Jota, aliyefariki dunia ajalini.
Mambo yameanza vizuri, ushindi kwenye mechi tatu mfululizo kwenye Ligi Kuu England ikizichapa Bournemouth, Newcastle na Arsenal, huku Ekitike akifunga kwenye mechi mbili za kwanza. Lakini, kiwango cha jumla cha Liverpoool bado kuna kitu cha kufanyika, huku ushindi wao kwenye mechi ya Arsenal ulitokana na bao la mpira wa adhabu wa Dominik Szoboszlai.
Salah alifunga dhidi ya Bournemouth na aliasisti pia bao la Rio Ngumoha kwenye ushindi uwanjani St James’ Park, lakini bado hajaanza kuonyesha yale makali yake.
Salah alisema bado hajapata muunganiko mzuri na mshambuliaji mwenzake, Ekitike.
“Hadi sasa bado hatujapata muunganiko mzuri,” alisema Salah.
“Kama ilivyokuwa kipindi cha Darwin au Lucho au watu wengine niliokuwa nacheza nao mbele au Diogo. Nilijua nianzie wapi ninapocheza na Diogo au Darwin. Nilijua namna ya kuwapasia. Nilifahamu mchezo wao vizuri sana, lakini sasa kwa huyu Hugo bado sijamfahamu vyema.”