Mo Salah aweka rekodi nyingine EPL
Muktasari:
- Staa huyu wa kimataifa wa Misri amefikia rekodi hiyo baada ya kufanya hivyo katika mchezo wa Jumatano dhidi ya Aston Villa wa sare ya mabao 2-2.
LIVERPOOL, ENGLAND: STAA wa Liverpool, Mohamed Salah ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga na kutoa pasi katika michezo 10 au zaidi kwenye ligi kwa simu mmoja baada ya Lionel Messi aliyefanya hivyo msimu wa 2014/15.
Staa huyu wa kimataifa wa Misri amefikia rekodi hiyo baada ya kufanya hivyo katika mchezo wa Jumatano dhidi ya Aston Villa wa sare ya mabao 2-2.
Rekodi hii iliwekwa na Messi akisaidiana na Suarez na Neymar wakati wapo Barcelona.
Kwa mujibu wa tovuti ya OptaJoe, Messi alifunga na kutoa pasi katika michezo 11 msimu huo, rekodi ambayo inakaribiwa na Salah ikiwa atafanya hivyo katika mchezo mmoja ujao.
Hadi sasa mshambuliaji huyu ana mabao 24 na pasi 15 katika michezo 26 ya Ligi Kuu England, pamoja na mabao matatu na pasi nne katika mechi saba za Ligi ya Mabingwa msimu huu.
Hii siyo rekodi pekee ambayo Salah aliiweka katika mchezo dhidi ya Villa, pia bao lake alilofunga ambalo ni la 29 kijumla msimu huu katika mashindano yote, lilikuwa ni bao lake la 15 kufunga katika mechi za ugenini, hali iliyomfanya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga mabao mengi ya ugenini katika msimu mmoja wa Ligi Kuu, awali, Luis Suarez alikua akishikilia rekodi hiyo akiwa na mabao 14 ya mechi za ugenini msimu wa 2013/14.