Martinez: tuwasaidie Hojlund, Zirkzee
Muktasari:
- Martinez amekiri timu inapaswa kufanya kazi ya ziada kuwasaidia washambuliaji wao Rasmus Hojlund na Joshua Zirkzee ambao kwa sasa wanakutana na wakati mgumu kwenye fowadi hiyo ya kikosi cha Ruben Amorim.
MANCHESTER, ENGLAND: BEKI wa kati wa Manchester United, Lisandro Martinez amewaambia wachezaji wenzake waache kuwapigia mipira mirefu mastraika wao.
Martinez amekiri timu inapaswa kufanya kazi ya ziada kuwasaidia washambuliaji wao Rasmus Hojlund na Joshua Zirkzee ambao kwa sasa wanakutana na wakati mgumu kwenye fowadi hiyo ya kikosi cha Ruben Amorim.
Martinez, ambaye alifunga bao la ushindi Jumapili iliyopita Man United ilipoichapa Fulham 1-0 Ligi Kuu England na kumshusha presha kocha Amorim, amekubali huduma wanayopewa washambuliaji wao Hojlund na Zirkzee haina viwango vya kutosha.
Alisema: “Lazima tukubali kuwajibika. Nadhani tunawapigia mipira mirefu sana ambayo kwao ni shida. Wanachuana na mabeki wawili wa kati na mabeki wawili Ligi Kuu England ni ngumu sana kucheza nao kwenye kugombea mipira.
“Lakini, nao wanapaswa kufanya vizuri pia. Ni wachezaji wazuri sana, lakini tunapaswa kuwasaidia sana ili kuwaweka kwenye nafasi nzuri. Tunawatafutie sehemu sahihi ya kuwaweka na kumweka eneo la hatari ili kuwasaidia kufunga.”
Hojlund, amefunga mara saba msimu huu, ameshindwa kufunga kwenye mechi 11 za mwisho.
Zirkzee amefunga mabao manne tangu alipojiunga na Man United kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana akitokea Bologna.
Man United kwa sasa inajiandaa na mchezo wa Europa League utakaopigwa kesho Alhamisi dhidi ya FCSB huko Romania ikienda kufukuzia ushindi wao wa tatu mfululizo chini ya kocha Amorim. Na Martinez alisema: “Yatupasa kuendelea na huu moto hakika. Ni hisia nzuri sana unaposhinda, lakini tuwe watulivu.”