Liverpool wanauliza, bado ngapi?

Muktasari:
- Ushindi huo umeifanya Liverpool kufikisha pointi 70 na inahitaji kushinda mechi sita tu zijazo ili kutangazwa kuwa mabingwa wa msimu huu.
LIVERPOOL, ENGLAND: HESABU za ubingwa kwa Majogoo wa Jiji la Liverpool zinatoa matumaini katika kutwaa taji la Ligi Kuu England msimu huu baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Southampton juzi Jumamosi.
Ushindi huo umeifanya Liverpool kufikisha pointi 70 na inahitaji kushinda mechi sita tu zijazo ili kutangazwa kuwa mabingwa wa msimu huu.
Kwa sasa inaongoza kwa tofauti ya pointi 16 baada ya mechi 29 huku wapinzani wao wakubwa kwenye mbio hizo, Arsenal iliyopo nafasi ya pili ina mechi mbili mkononi.
Hata hivyo, sasa majogoo hawa wanajua ni pointi ngapi wanahitaji kuhakikisha wanapata taji la ligi msimu huu.
Kiujumla vigogo hawa wanahitaji pointi 18 zaidi ili kuhakikisha wanapata taji ambao ni sawa na kushinda mechi sita zijazo hata kama Arsenal ikishinda mechi zao zote zilizobakia.
Ikiwa Arsenal itashinda mechi zote zilizobakia itafikisha a pointi 87, wakati Liverpool ikishinda mechi sita zijazo itakusanya jumla ya alama 88.
Kampeni yao ya kushinda mechi sita itaanzia mwezi ujao ambapo watacheza dhidi ya Everton katika dimba la Anfield April 02 baada ya Mapumziko ya kupisha kalenda ya FIFA.
Baada ya hapo wataumana na Fulham ugenini April 6 kisha West Ham nyumbani April 13, kisha watasafiri kwenda jijini Leicester kuvaana na Leicester City na baadae wataikaribisha Tottenham ya Ange Postecoglou Anfiled.
Mchezo wa sita ambao watatakiwa kushinda baada ya kushinda mitano ya hapi juu ni dhidi ya Chelsea ambao utapigwa Mei 03 katika dimba la Stamford Bridge.
Hata hivyo, kuna uwezekano wasishinde mechi hizo sita kwani na wakachukua ubingwa kwa kushinda tano au nne ingawa hiyo itategemea na matokeo ambayo Arsenal itakuwa inayapata.