Lescott: Kwa Isak? Ekitike ni benchi tu
Muktasari:
- Staa wa Sweden, Isak amekamilisha uhamisho wake wa kujiunga na Liverpool kwa ada iliyovunja rekodi huko Uingereza ya Pauni 130 milioni kutoka Newcastle United.
LIVERPOOL, ENGLAND: BEKI wa zamani wa Manchester City na England, Joleon Lescott anaamini kocha wa Liverpool, Arne Slot atamweka benchi Hugo Ekitike ili kumwanzisha straika, Alexander Isak.
Staa wa Sweden, Isak amekamilisha uhamisho wake wa kujiunga na Liverpool kwa ada iliyovunja rekodi huko Uingereza ya Pauni 130 milioni kutoka Newcastle United.
Sakata lake la usajili lilitumia muda mrefu kukamilika na baada ya uhamisho wake umeifanya Liverpool kufanya matumizi yanayozidi Pauni 400 milioni kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka huu, huku straika Mfaransa, Ekitike naye alinaswa kwa pesa nyingi, Pauni 79 milioni kutokea Frankfurt ya Ujerumani.
Ekitike ameanza maisha yake vizuri huko Merseyside, akifunga kwenye mechi ya kipigo kwa Liverpool katika Ngao ya Jamii na alifunga kwenye mechi mbili za kwanza za Ligi Kuu England.
Lakini, Lescott anaamini fowadi huyo Mfaransa atasugua benchi baada ya ujio wa Isak kwenye kikosi hicho cha Anfield, huku kushoto na kulia kwenye fowadi ya Liverpool, kocha Slot atakuwa na huduma ya Mohamed Salah na Cody Gakpo.
"Ekitike anaweza kuwa benchi Liverpool. Itabidi akae huko," alisema Lescott.
"Tuliona vitu kama hivyo vikitokea kwa timu nyingine. Julian Alvarez alikaa benchi na kuingia kufunga mabao nyuma ya Erling Haaland huko Manchester City."
Lescott anaamini kocha Slot anaweza pia kuchagua namna ya kuwatumia washambuliaji wake hao kwa kuwabadilishabadilisha kulingana na mechi zitakazowakabili.