Kompany atoa neno jeraha la Kane
Muktasari:
- Katika dakika ya 60 ya mechi hiyo ya Bundesliga iliyochezwa nyumbani kwa Borussia Dortmund na kumalizika kwa sare ya 1-1, mchezaji huyo wa kimataifa wa England alilazimika kutoka nje kwa kilichoonekana majeraha ya paja.
MUNICH, UJERUMANI: KOCHA wa Bayern Munich, Vincent Kompany ametoa dokezo kuhusu hali ya Harry Kane baada ya straika huyo kuumia na kutoka nje wakati wa mechi dhidi ya Borussia Dortmund.
Katika dakika ya 60 ya mechi hiyo ya Bundesliga iliyochezwa nyumbani kwa Borussia Dortmund na kumalizika kwa sare ya 1-1, mchezaji huyo wa kimataifa wa England alilazimika kutoka nje kwa kilichoonekana majeraha ya paja.
Baada ya mechi hiyo, kocha Kompany alisema aliona hofu iliyomjaa Kane baada ya jeraha hilo lakini anatarajia mazuri kwa staa huyo mwenye umri wa miaka 31.
Kompany alisema: “Harry alisema hajaumia sana. Natumai itakuwa hivyo. Tusubiri tutaona majibu wa vipimo. Lakini niliihisi hofu aliyokuwa nayo baada ya kuumia...”
“Itakuwa ngumu. Siwafahamu wachezaji wengi ambao wameweza kupona haraka katika kipindi kifupi kiasi hicho. Tutajua vizuri baadaye.
“Hakika mabao ya Harry ni ngumu kuyapatia mbadala, lakini tulisema kutokea mwanzo tunaiamini timu. Tulitengeneza nafasi nyingi kipindi cha pili. Timu imejaa vipaji katika kushambulia. Ni ngumu kumpata mbadala wa Harry, lakini tunaweza kulitatua hilo kwa kuwatumia wachezaji wengine tulionao kikosini.”
Wenyeji walipata bao katika dakika ya 27 pale Gittens alipokimbia na mpira mita 45 na kumtungua Manuel Neuer, kabla ya mtokea benchini Jamal Musiala kuisawazishia Bayern katika dakika ya 85 akiunganisha krosi ya Michael Olisse.