Kocha Sweden amtetea Isak
Muktasari:
- Straika Isak alikosa mechi ya kwanza ya Ligi Kuu England dhidi ya Aston Villa msimu huu akipambana kulazimisha uhamisho wa kwenda Liverpool.
STOCKHOLM, SWEDEN: KOCHA wa Sweden, Jon Dahl Tomasson amewaonya watu waache kumhukumu Alexander Isak kwa sababu hawafahamu kiundani juu ya sakata lake kwenye klabu ya Newcastle United.
Straika Isak alikosa mechi ya kwanza ya Ligi Kuu England dhidi ya Aston Villa msimu huu akipambana kulazimisha uhamisho wa kwenda Liverpool.
Staa huyo amekuwa akifanya mazoezi kivyake baada ya kutokuwamo kwenye kikosi cha Newcastle kilichokuwa kwenye pre-season huko Asia na kilichoonekana awali ni kama vile ameshamaliza kuichezea timu hiyo.
Hata hivyo, kocha wa Newcastle United, Eddie Howe ameacha milango wazi kwa straika huyo kurejea kwenye kikosi licha ya kwamba amejiweka mbali.
Liverpool ilipeleka ofa ya Pauni 110 milioni kwa ajili ya kunasa huduma ya mshambuliaji huyo, lakini Newcastle imegomea ofa hiyo, huku ikisisitiza mchezaji huyo hauzwi.
Dirisha la usajili bado halijafungwa na Liverpool bado ina matumaini makubwa ya kumsajili mshambuliaji huyo ili kwenda kuboresha makali Anfield.
Baada ya Isak kuonekana kama anakosea kwa uamuzi wake wa kujiweka mbali na kikosi cha Newcastle, kocha wa timu yake ya taifa, Tomasson ameibuka kumtetea. Kocha huyo wa Sweden katika dirisha hili la majira ya kiangazi alimshuhudia straika wake mwingine, Viktor Gyokeres akiigomea Sporting Lisbon kulazimisha uhamisho wa kwenda kujiunga na Arsenal.
Tomasson anaamini wakosoaji hawapaswi kuzungumza sana kabla ya kupata ukweli wote wa kuhusu mazingira yanayosababisha Isak kutaka kuondoka kwenye kikosi hicho cha St James' Park.