James Maddison nje wiki kibao Spurs
Muktasari:
- Staa huyo wa kimataifa wa England aliumia kwenye mechi ya pre-season na baada ya kubainika kuumia misuli ya goti, atahitaji kufanyiwa upasuaji.
LONDON, ENGLAND: KIUNGO mchezeshaji wa Tottenham Hotspur, James Maddison atakosa sehemu kubwa ya msimu baada ya kupata maumivu makubwa ya goti.
Staa huyo wa kimataifa wa England aliumia kwenye mechi ya pre-season na baada ya kubainika kuumia misuli ya goti, atahitaji kufanyiwa upasuaji.
Mchezaji mwingine wa Ligi Kuu England aliyewahi kupata maumivu kama hayo, kiungo wa Rodri alikuwa nje ya uwanja kwa miezi minane na kushindwa kuitumikia timu yake kwa msimu uliopita.
Maddison aliumia wakati akiitumikia Spurs kwenye mechi ya pre-season dhidi ya Newcastle na hivyo kulazimika kutolewa uwanjani kwa machela.
Kocha wa Spurs, Thomas Frank alisema kwamba majeraha hayo amepata kwenye goti lilelile lililomfanya akose fainali ya Europa League dhidi ya Manchester United, Mei mwaka huu.
“Tunathibitisha kwamba James Maddison atafanyiwa upasuaji baada ya kuumia goti la mguu wa kulia,” ilibainisha taarifa ya Spurs.
“Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 28 aliumia kwenye mechi yetu ya kirafiki dhidi ya Newcastle United, Jumapili mjini Seoul. Upasuaji wake utafanyika siku chache zijazo na kutokana na hilo, James atalazimika kuwa nje kujiuguza.
“Kila mtu wa Tottenham Hotspur anamtakia James heri na apone haraka. Tutamsapoti kwa kila hatua.”
Frank alisema baada ya mechi hiyo ya Newcastle: “Ni goti lilelile alilokuwa amejiumiza huko nyuma.”
Spurs sasa inatarajia kuingia sokoni kutafuta mbadala wake huku wachezaji Morgan Gibbs-White na Ebere Eze wakiwahi kuhusishwa na miamba hiyo sambamba na Harvey Elliott wa Liverpool.