Isak afunguka kutua Anfield
Muktasari:
- Staa huyo wa kimataifa wa Sweden alikamilisha uhamisho wa kujiunga na Liverpool baada ya muda mrefu, ambapo miamba hiyo ya Anfield imekubali kulipa Pauni 130 milioni kunasa saini yake kutoka Newcastle United.
LIVERPOOL, ENGLAND: STRAIKA Alexander Isak amesema isingekuwa rahisi kukomea nafasi ya kujiunga na Liverpool kwa ada inayovunja rekodi ya uhamisho England huku akitambua hilo limefikisha mwisho wasiwasi uliokuwa umezingira hatima ya soka lake.
Staa huyo wa kimataifa wa Sweden alikamilisha uhamisho wa kujiunga na Liverpool baada ya muda mrefu, ambapo miamba hiyo ya Anfield imekubali kulipa Pauni 130 milioni kunasa saini yake kutoka Newcastle United.
Kitendo cha kulazimisha uhamisho huo, Isak amejitengenezea uadui mkubwa kwa mashabiki wa Newcastle United. Lakini, hata hajali na sasa anasubiria uanza kuwatumikia waajiri wake wapya, ambapo wamemkabidhi jezi Namba 9.
Alipoulizwa kwanini Liverpool ndio aliona ni sehemu sahihi ya kwenda, Isak alisema: “Ni mchanganyiko wa namna klabu ilivyojengwa, lakini zaidi ni ukubwa wa klabu ambao tayari umefikia. Historia ya klabu. Mimi kupata nafasi ya kuwa sehemu hiyo, nilitaka kutengeneza historia. Nataka kushinda mataji pia.
“Hilo limenichochea zaidi na nadhani hapa ni mahali sahihi pa kukuza soka langu na kupandisha viwango. Najiona kama nimepiga hatua ya juu kwenye maisha yangu ya soka. Nimefurahi sana kwa kupewa nafasi hii na nahamasika kufanya mambo mazuri zaidi.” Isak alifunga mabao 62 kwenye kikosi cha Newcastle United kwa misimu mitatu aliyotumia timu hiyo na alifunga mara mbili wakati alipokabiliana na Liverpool uwanjani Anfield kipindi hicho alipokuwa akivaa jezi nyeusi na nyeupe.