He! Mabosi Sporting wamtibua Gyokeres

Muktasari:
- Fowadi huyo wa Sweden amekuwa lulu akisakwa na timu nyingi kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi baada ya kufanya vizuri kwa msimu wa pili mfululizo akiwa na miamba hiyo ya Ureno.
LISBON, URENO: STRAIKA wa mabao, Viktor Gyokeres ameripotiwa kuwakasirikia mabosi wa Sporting Lisbon baada ya kufanya mabadiliko kwenye kipengele kinachotaja bei anayouzwa mshambuliaji huyo.
Fowadi huyo wa Sweden amekuwa lulu akisakwa na timu nyingi kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi baada ya kufanya vizuri kwa msimu wa pili mfululizo akiwa na miamba hiyo ya Ureno.
Gyokeres inaripotiwa alifikia makubaliano na mabosi wa klabu yake mwanzoni mwa msimu huu na ataruhusiwa kuondoka kwa ada isiyozidi Pauni 84 milioni, kwamba ni kipengele kilichochomekwa kwenye mkataba wake. Na kwenye hilo, fowadi huyo mwenye umri wa miaka 27, aliambiwa ataondoka kwa ada ya jumla ya Pauni 59 milioni na Pauni 51 milioni itapaswa kutangua kulipwa.
Lakini, gazeti moja la Ureno, Record limedai Sporting imebadili mawazo na haiwezi kuachana na Gyokeres la kama tu italipwa Pauni 67 milioni.
Gyokeres, ambaye anasakwa na Manchester United, anaripotiwa kukasirishwa na uamuzi huo wa klabu akieleza amesalitiwa. Straika huyo anataka kuondoka Sporting dirisha hili na miamba miwili ya Ligi Kuu England, Man United na Arsenal inachuana kuwania saini yake.
Alifunga mabao 54 na asisti 13 katika mechi 52 alizocheza msimu uliopita na hivyo kumfanya awe ameifungia klabu hiyo mabao 97 katika mechi 102.
Kama Man United italipa Pauni 67 milioni, Gyokeres atakuwa na nafasi ya kwenda kukutana na kocha wake wa zamani Ruben Amorim huko Old Trafford.