Harry Kane aifikia rekodi ya Ronaldo UEFA
Muktasari:
- Kane sasa amekuwa mchezaji wa pili pekee katika historia kufunga katika mechi sita mfululizo za hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, akiifikia rekodi iliyowekwa na Ronaldo kati ya mwaka 2012 na 2013.
MUNICH, UJERUMANI: STAA wa Bayern Munich na England, Harry Kane ameifikia rekodi ya kipekee ya Cristiano Ronaldo katika Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kufunga katika mechi sita mfululizo za hatua ya mtoano.
Kane ambaye alifunga katika mechi ya nusu fainali juzi dhidi ya PSG, bao lake la kihistoria halikutosha kuiokoa Bayern na janga la kuondoshwa mashindanoni baada ya matokeo ya jumla kuwa ni mabao 6-5, hivyo watoto wa Paris wakatinga fainali na watacheza dhidi ya Arsenal.
Kane sasa amekuwa mchezaji wa pili pekee katika historia kufunga katika mechi sita mfululizo za hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, akiifikia rekodi iliyowekwa na Ronaldo kati ya mwaka 2012 na 2013.
Straika huyo wa England alifunga bao muhimu dakika ya 94 katika sare ya 1-1 dhidi ya mabingwa watetezi Paris Saint-Germain kwenye Uwanja wa Allianz Arena.
Licha ya juhudi zake za mwisho pamoja na penalti aliyofunga katika kipigo cha mabao 5-4 kwenye mechi ya mkondo wa kwanza, Bayern ilitolewa kwa maumivu makubwa.
Mabingwa hao wa Ujerumani waliaga mashindano kwa jumla ya mabao 6-5 na kuwaacha PSG wakisonga mbele hadi fainali.
Kane aliondoka Tottenham Hotspur, klabu yake ya utotoni, na kujiunga na Bayern akiwa na lengo kuu la kutwaa mataji makubwa ya Ulaya.
Ingawa Bayern walifika hatua ya nusu fainali msimu huu baada ya kutolewa robo fainali katika misimu miwili iliyopita, bado taji kubwa limeendelea kuwa ndoto ngumu kwa mshambuliaji huyo mwenye mabao mengi.
Kane aliwahi kucheza fainali moja tu ya Ligi ya Mabingwa akiwa Tottenham, ambapo walipoteza dhidi ya Liverpool.
Licha ya kuwa na msimu bora binafsi akiwa amefunga mabao 56 katika mechi 49, sasa atalazimika kusubiri takribani miezi tisa kabla ya kuanza tena safari yake ya kutafuta medali ya ubingwa wa taji hilo.
Hata hivyo, hadi kufikia sasa Bayern wameshatangazwa kuwa mabingwa wa Bundesliga, huku wakiwa wamebakiwa na mechi mbili mkononi.
Vilevile, wapo katika fainali ya DFB-Pokal na watacheza dhidi ya Stuttgart Mei 23.