Harden aweka rekodi ya hovyo NBA
Muktasari:
- Lakini sasa, kadri miaka inavyosogea na presha ya kutafuta ubingwa wa NBA ikizidi kuongezeka, nyota huyo ameanza kutajwa kwa rekodi za aibu zinazotia doa kwenye historia yake.
CLEVELAND, MAREKANI: KWA miaka mingi, James Harden amekuwa akitajwa sambamba na ubora mkubwa wa kufunga, uwezo wa kutengeneza nafasi na kuwa mmoja wa mastaa waliotikisa zaidi mchezo wa mpira wa kikapu duniani.
Lakini sasa, kadri miaka inavyosogea na presha ya kutafuta ubingwa wa NBA ikizidi kuongezeka, nyota huyo ameanza kutajwa kwa rekodi za aibu zinazotia doa kwenye historia yake.
Katika kipindi ambacho Cleveland Cavaliers walihitaji uzoefu na ubora wake zaidi kuliko wakati mwingine wowote, Harden alionekana kivuli cha mchezaji aliyewahi kuitikisa NBA akiwa Houston Rockets.
Cavaliers walijikuta wakipokea kipigo cha pointi 107-97 kutoka kwa Detroit Pistons katika mchezo wa pili wa nusu fainali ya Ukanda wa Mashariki, matokeo yaliyowaweka katika wakati mgumu sana wa kusaka nafasi ya kutinga hatua inayofuata ya mchujo.
Hata hivyo, pamoja na kipigo hicho, mjadala mkubwa zaidi uliibuka kuhusu kiwango kibovu cha Harden ambaye alishindwa kabisa kuibeba timu yake katika usiku ambao ulitakiwa kuwa wake.
Nyota huyo mwenye miaka 36 alipiga mitupio 13 lakini akaambulia kufunga mitatu pekee huku akishindwa kabisa kufunga hata mpira mmoja wa pointi tatu kati ya minne aliyojaribu.
Harden alimaliza mchezo akiwa na pointi 10, rebound sita, pasi tatu za mwisho na kuiba mpira mmoja, takwimu ambazo ziliwaacha wengi wakishangaa kama bado ana uwezo wa kuwa msaada katika michezo mikubwa.
Kilichowaumiza zaidi mashabiki wa Cavaliers ni namna Harden alivyopotea kabisa kipindi cha pili cha mchezo. Kati ya pointi zake zote 10, mbili pekee ndizo alizofunga katika nusu ya pili, wakati Pistons wakizidi kuimarika na kuutawala mchezo. Kwa mchezaji aliyewahi kuwa MVP wa NBA na mmoja wa wafungaji bora wa kizazi chake, kiwango hicho kilionekana kuwa cha kawaida mno na kisichoendana na ukubwa wa jina lake.
Mbaya zaidi, mchezo huo ulimfanya Harden kuvunja rekodi mbaya iliyokuwa imedumu kwa zaidi ya miaka 70.
Kwa mujibu wa takwimu za ESPN, sasa Harden ana michezo 20 ya mchujo kabla ya mechi ya leo, Jumapili aliyopiga chini ya asilimia 25 ya mitupio yake akiwa amejaribu angalau mara 10, rekodi mbaya zaidi tangu kuanzishwa kwa mfumo wa ‘shot-clock’ 1954/55.
Kwa kufanya hivyo, alimzidi gwiji wa zamani wa Boston Celtics, Bob Cousy ambaye alikuwa ameshikilia rekodi hiyo kwa miongo kadhaa. Takwimu hizo zimezidisha mjadala kuhusu uwezo wa Harden katika michezo ya mchujo, eneo ambalo limekuwa likimwandama kwa miaka mingi licha ya mafanikio yake makubwa msimu wa kawaida.
Katika maisha yake yote ya mchujo akiwa amecheza michezo 182, huu ulikuwa mchezo wa 36 kwa Harden kufunga mitupio mitatu au chini ya hapo. Hiyo ina maana karibu asilimia 20 ya michezo yake ya mchujo imekuwa ya kiwango cha chini kwa upande wa ufungaji.
Mbali na hilo, Harden pia ameendelea kuwa tatizo kwa upande wa kupoteza mipira. Katika mchezo huo dhidi ya Pistons, alikuwa tena na ‘turnovers’ nyingi kuliko mitupio aliyofunga, jambo lililoifanya iwe mara ya 46 kwake kufanya hivyo katika mchujo.
Kwa lugha nyingine, zaidi ya robo ya michezo yake yote ya mchujo imekuwa ikihusisha Harden kupoteza mipira kwa kiwango kinachoumiza timu yake.
Katika michezo miwili ya kwanza ya mfululizo huo dhidi ya Pistons, Harden ana wastani wa pointi 16 pekee huku akitupia asilimia 32.1 kutoka uwanjani na asilimia 9.1 katika mipira ya pointi tatu, kiwango ambacho hakijawahi kutarajiwa kutoka kwa mchezaji mwenye historia yake. Licha ya lawama zote hizo, staa mwenzake Donovan Mitchell ameendelea kumuamini Harden na kusisitiza kuwa bado ana nafasi ya kubadilisha hali.
“Yeye ni James Harden. Hatuna sababu ya kuanza kuwa na hofu. Wachezaji wakubwa hupitia nyakati kama hizi lakini wana uwezo wa kurejea,” alisema Mitchell. Kauli hiyo ya Mitchell imeonekana kuwa jaribio la kupunguza presha inayomkabili Harden, lakini wachambuzi wengi wa NBA hawaonekani kuwa tayari kumpa muda zaidi.
Bingwa mara tatu wa NBA, Udonis Haslem alimkosoa Harden akisema kinachotokea hakiendani kabisa na uzoefu wake mkubwa ndani ya mchezo.
Haslem alisema mchezaji ambaye amecheza hatua ya mchujo kwa miaka 17 mfululizo anapaswa kuwa mtulivu zaidi badala ya kufanya makosa mepesi yanayoigharimu timu. “Unawezaje kupoteza mipira kirahisi hivyo wakati umecheza hatua hizi kwa miaka mingi? Haya ni makosa ambayo hata watoto wadogo wakifanya unaweza kuwatoa nje ya mchezo,” alisema Haslem.
Kauli hizo zilionyesha wazi namna ambavyo watu wengi ndani ya NBA wameanza kuchoshwa na mwenendo wa Harden katika mchujo. Mchezaji mwingine wa zamani wa NBA, Kendrick Perkins naye alikoleza moto akisema Harden kwa sasa amekuwa mzigo kwa Cavaliers.
Perkins alisema Harden hafanyi kazi ya ulinzi, hashambulii kwa ufanisi na pia anapoteza mipira mingi, jambo ambalo linaifanya timu yake kupata shida kubwa kila anapokuwa uwanjani kwa muda mrefu.
Kocha wa Cavaliers, Kenny Atkinson amekuwa akimtumia Harden wastani wa dakika 35.1 kwa kila mchezo, muda mkubwa zaidi ndani ya kikosi hicho, lakini sasa kuna presha kubwa kwake kufanya mabadiliko kabla hali haijawa mbaya zaidi.