Gyokeres kupewa namba ya Henry
Muktasari:
- Hiyo ina maana, Gyokeres atavaa jezi yenye Namba 14, ambayo ni maarufu sana kwenye kikosi cha Arsenal, ambayo kwa sasa ameirithi kwa Eddie Nketiah.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL imekubali rasmi kumsajili straika Viktor Gyokeres kutoka Sporting Lisbon na kumkabidhi staa huyo jezi iliyokuwa ikivaliwa na gwiji Thierry Henry.
Hiyo ina maana, Gyokeres atavaa jezi yenye Namba 14, ambayo ni maarufu sana kwenye kikosi cha Arsenal, ambayo kwa sasa ameirithi kwa Eddie Nketiah.
Kocha Mikel Arteta anamtaka straika huyo kwenda kuungana na wachezaji wenzake kwenye kambi ya pre-season huko Singapore na Hong Kong.
Straika Gyokeres, 27, alitarajia kusafiri kutoka Ureno kwenda London jana Jumamosi kwenda kukamilisha vipimo vya afya baada ya kukubali dili la mkataba wa miaka mitano wa kuichezea Arsenal. Kuhusu ada ya uhamisho, Arsenal itatanguliza kulipa Pauni 54.8 milioni kisha italipa bonasi ya Pauni 8.7 milioni kulingana na kiwango chake cha uwanjani ikiwamo kufunga mabao 20 au zaidi na timu ikifuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya. Jambo hilo litafanya matumizi ya Arsenal kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi kuzidi Pauni 200 milioni baada ya kuwanasa pia Martin Zubimendi, Kepa Arrizabalaga, Christian Norgaard, Noni Madueke na Cristhian Mosquera.
Arsenal itakipiga na Newcastle, Jumapili huko Singapore na mechi hiyo itakuwa mapema sana kwa Gyokeres kucheza, lakini matarajio makubwa kwamba atakuwapo uwanjani kuwatazama wachezaji wenzake wakicheza.
Na kama mpango utakwenda vizuri, mechi yake ya kwanza itakuwa Hong Kong wakati Arsenal itakapokabiliana na mahasimu wao wa North London, Tottenham Hotspur, Alhamisi.