Gabriel bado yupo sana Arsenal

Muktasari:
- Gabriel Magalhaes alijiunga na Arsenal mwaka 2020 akitokea Lille inayoshiriki Ligi Kuu ya Ufaransa.
LONDON, ENGLAND: Beki wa Kati raia wa Brazil, Gabriel Magalhaes (27) ameongeza mkataba wa kuitumikia Arsenal hadi 2029.
Mkataba wa awali wa mchezaji huyo ulikuwa ufikie tamati Julai 2027 lakini kutokana na umuhimu wake kikosini, timu hiyo imeamua kumpa mkataba mrefu zaidi wa kuendelea kuitumikia.
Mlinzi huyo wa kati amekuwa tegemeo la Arsenal tangu alipojiunga nayo kwa uhamisho wa Pauni 27 milioni kutoka Lille ya Ufaransa, mwaka 2020 ambapo tangu hapo hadi sasa, ameichezea Arsenal mechi 210 za mashindano tofauti.
Muda mfupi baada ya kusaini mkataba huo mpya, Magalhaes amesema kuwa amefanya hivyo kutokana na mapenzi aliyonayo kwa Arsenal.
“Niliwasili hapa nikiwa kijana mdogo na baada ya miaka mitano nina furaha sana na nimejifunza mengi.
Nina fahari kwa ajili yangu. Ni safari ya kipekee na nina furaha kuiendeleza. Natumaini nitashinda baadhi ya mataji na klabu hii kwa sababu ninaipenda na familia yangu inaipenda klabu hii pia.
“Arsenal ni klabu ya kipekee na nina fahari kusaini mkataba mpya. Ninawapenda mashabiki, wenzangu tuliopo kwenye timu, naupenda uwanja. Nina fahari na nashukuru kwa sapoti yote. Tunaendelea pamoja kwa ajili ya baadaye,” amesema Magalhaes.
Tangu 2022, Magalhaes ametengeneza pacha imara ya ulinzi na beki mwingine wa kati wa timu hiyo, William Saliba.
Pacha hiyo imeonekana kuwapa kazi ngumu washambuliaji wa timu pinzani kuipita na kuthibitisha hilo katika misimu miwili mfululizo iliyopita kwenye Ligi Kuu England (EPL), Arsenal imeongoza kwa kuruhusu idadi ndogo ya mabao.