Duh! Timu yakimbia mechi Uturuki
Muktasari:
- Mechi hiyo ya Ligi Kuu Uturuki kwanza ilisimama baada ya dakika 34 kufuatia vinara Galatasaray kuongoza bao 1-0.
ISTANBUL, UTURUKI: MECHI ya Galatasaray kwenye Super Lig dhidi ya Adana Demirspor imevunjika baada ya timu ya ugenini kugoma kuendelea na mchezo.
Mechi hiyo ya Ligi Kuu Uturuki kwanza ilisimama baada ya dakika 34 kufuatia vinara Galatasaray kuongoza bao 1-0.
Alvaro Morata aliifungia bao la kuongoza Galatasaray kwa mkwaju wa penalti katika kipute hicho cha uwanjani Rams Park baada ya dakika ya 12 tu.
Dries Mertens aliangushwa ndani ya boksi na beki wa Adana, na kuamriwa kupigwa mkwaju wa penalti uliowekwa kimiani na Morata - ambaye anacheza kwa mkopo kwenye timu hiyo akitokea AC Milan - hivyo kufunga bao lake la pili katika mechi tatu alizochezea Galatasaray.
Kocha wa Adana, Mustafa Alper Avci alionekana akiwaita wachezaji wake pembeni ya uwanja wakati kiungo Yusuf Barasi alipokuwa akipatiwa matibabu baada ya kuumia. Lakini, ghafla tu wachezaji wa timu hiyo inayoshika mkia kwenye msimamo wa Super Lig waliamua kutoka uwanjani na kuingia vyumbani.
Jambo hilo liliwashangaza wachezaji wa Galatasaray pamoja na waamuzi wa mchezo na baada ya mechi kusimama kwa zaidi ya dakika 20, mtangazaaji wa uwanjani alitangaza mechi hiyo kuvunjika.
Mtangazaji huyo alisikika akiwema: "Mechi imevunjwa na mwamuzi baada ya Adana Demirspor kujitoa kwenye mchezo."
Rais wa zamani wa klabu ya Adana Demirspor, Metin Korkmaz, alithibitisha kwamba uamuzi huo ulikuwa ni mgomo dhidi ya penalti hiyo ya mapema.
Alisema: "Huu ulikuwa ni mgomo dhidi ya kamati ya waamuzi na sio Galatasaray."