Duh! Sikia hii ya Gyokeres
Muktasari:
- Beki huyo Mwingereza alimshangaza hata mchambuzi mwenzake beki wa zamani wa Manchester United, Gary Neville akipinga hayo.
LONDON, ENGLAND: BEKI wa zamani wa Liverpool, Jamie Carragher ameshangaza wengi kudai kocha Mikel Arteta hatamtumia straika mpya Viktor Gyokeres katika mechi kubwa za Arsenal msimu huu.
Beki huyo Mwingereza alimshangaza hata mchambuzi mwenzake beki wa zamani wa Manchester United, Gary Neville akipinga hayo.
Gyokeres alianzishwa kwenye mechi ya kwanza ya Arsenal ya ligi dhidi ya Manchester United na alicheza kwa dakika 60 kabla ya kutolewa. Straika huyo alishindwa kuonyesha makali, ambapo hakupiga shuti kulenga goli muda wote, licha ya Arsenal ilipata ushindi wa bao 1-0 Old Trafford.
Na katika kuhakikisha kikosi kinafanya vizuri, Carragher anaamini Arteta hatamtumia Gyokeres kwenye mechi ngumu za kupambana na timu kama Chelsea, Liverpool, Manchester City, Man United na Tottenham, huku rekodi zikionyesha The Gunners haijapoteza mechi kati ya 22 ilizocheza dhidi ya timu hizo kubwa. Carragher alisema haamini Gyokeres kama atashindwa kufunga mabao, lakini Kai Havertz ni muhimu katika mechi kubwa.
“Kama nitaamua kusema ukweli, nadhani watamrudi kwa Havertz kwenye mechi kubwa, naamini itakuwa hivyo,” alisema Carragher.
Neville alijibu: “Hawezi kumweka nje Gyokeres kwenye mechi kubwa.” Lakini, Carragher alidakia haraka na kusema: “Anaweza. “Nadhani Havertz ni mchezaji muhimu kwa Mikel Arteta kuendelea kumwaacha nje. Sioni hilo likitokea.”
Neville alitoa maoni ya mastaa hao wote wawili kucheza kwa pamoja aliposema: “Arsenal ilihitaji mshambuliaji wa kati na imemsajili, hivyo nadhani atamtumia sana. Nadhani Gyokeres na Havertz kucheza pamoja ni kitu kizuri.”