Duh! Kiungo Dani Olmo ang’oka jino uwanjani
Muktasari:
- Olmo, 26, alifanyiwa madhambi na Bartra dakika ya 30 katika kipute hicho kilichofanyika Uwanja wa Benito Villamarin.
BARCELONA, HISPANIA: KIUNGO wa Barcelona, Dani Olmo ameng’oka jino baada ya kugongana na beki wa Real Betis, Marc Bartra katika mchezo wa La Liga uliofanyika Jumamosi.
Olmo, 26, alifanyiwa madhambi na Bartra dakika ya 30 katika kipute hicho kilichofanyika Uwanja wa Benito Villamarin.
Baada ya kuchezewa rafu na beki huyo wa kati, Olmo alianguka na bahati mbaya alikwenda kujigonga kichwa kwenye kisigino cha mchezaji huyo.
Jambo hilo lilimfanya Olmo kung’oka jino na kuanza kulitafuta kwenye nyasi za uwanjani hapo. Bahati nzuri, Mhispaniola huyo aliliona jino lake lililong’oka haraka na kuonekana akiwa amehuzunishwa kwa jambo hilo wakati alipokuwa akimlalamikia mwamuzi kabla ya mechi kuendelea.
Mechi hiyo ilimalizika kwa timu hizo kufungana 2-2 baada ya Betis kusawazisha kwenye dakika za majeruhi kupitia kwa mkali Assane Diao.
Robert Lewandowski alifunga bao la kwanza kwa Barcelona kabla ya mapumziko akiwa ndani ya boksi. Staa wa zamani wa Tottenham, Giovani Lo Celso aliisawazishia Betis kwa mkwaju wa penalti, lakini Torres akawafungia bao jingine Barca katika dakika 10 za mwisho.
Katika dakika za majeruhi, Diao aliinusuru Betis kupata kipigo nyumbani baada ya kusawazisha na kufanya mechi hiyo kumalizika kwa sare ya 2-2. Matokeo hayo bado yanawafanya Barcelona kuendelea kushika usukani wa La Liga kwa kuwa na pointi 38, huku Betis ikibaki kwenye nafasi ya 11.