Bruno kama Rooney miaka 10 iliyopita
Muktasari:
- Mchezaji huyo ameshinda kwa tofauti ndogo dhidi ya nyota wa Arsenal, Declan Rice, akitwaa tuzo hiyo na kuwa mshindi wa kwanza wa klabu yake tangu 2010 ilipobebwa na Rooney kufuatia namba zake zinazotisha msimu huu kwenye ligi hiyo.
LONDON, ENGLAND: KIUNGO na nahodha wa Manchester United, Bruno Fernandes ameshinda kuwa Mchezaji Bora wa Mwaka wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezon England (FWA), ikiwa ni baada ya miaka 16 tangu aliyekuwa mshambuliaji wa kikosi hicho, Wayne Rooney aliponyakua tuzo hiyo.
Mchezaji huyo ameshinda kwa tofauti ndogo dhidi ya nyota wa Arsenal, Declan Rice, akitwaa tuzo hiyo na kuwa mshindi wa kwanza wa klabu yake tangu 2010 ilipobebwa na Rooney kufuatia namba zake zinazotisha msimu huu kwenye ligi hiyo.
Nahodha huyo wa United ametambuliwa kutokana na kiwango chake bora baada ya kutoa pasi 19 za mabao na kubaki moja kufikia rekodi ya Ligi Kuu England inayoshikiliwa na Thierry Henry na Kevin De Bruyne huku kukiwa na michezo mitatu imebakiwa.
Fernandes pia amefunga mabao manane na kuhusika moja kwa moja katika mabao 27, akiisaidia United kumaliza nafasi ya tatu na kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Nyota huyo kimataifa wa Ureno mwenye miaka 31 alikuwa mchezaji pekee wa United aliyeteuliwa akipata asilimia 45 ya kura kutoka kwa wanachama zaidi ya 900 wa FWA.
Katika ushindani mkali wa tuzo hiyo kongwe zaidi binafsi kwenye soka ambayo imekuwa ikitolewa tangu 1947, Fernandes alimzidi Rice kwa kura 28 huku mshambuliaji wa Manchester City, Erling Haaland akimaliza wa tatu. Kura za Arsenal ziligawanyika kwa Rice, David Raya, Gabriel Magalhaes na Bukayo Saka.
Kwa upande wa wanawake, Khadija ‘Bunny’ Shaw alishinda baada ya kuiongoza Manchester City kutwaa ubingwa wa kwanza wa Ligi Kuu ya Wanawake (WSL) ndani ya miaka 10 akiwa amefunga mabao 19 katika michezo 21. Shaw ambaye mkataba wake na City unaisha msimu huu, amefunga mabao 110 katika mechi 133 tangu ajiunge na klabu hiyo kutoka Bordeaux 2021.
Mshambuliaji huyo mwenye miaka 29 ambaye alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Wanawake 2024, aliwashinda Alessia Russo wa Arsenal na Lauren James wa Chelsea. Washindi watakabidhiwa tuzo zao katika hafla ya kila mwaka ya Footballer of the Year jijini London, Mei 19.
Mwenyekiti wa FWA John Cross alisema: “Wachezaji wote wawili wamekuwa na ushawishi mkubwa katika kiwango cha timu zao msimu huu. Pia ni mifano bora na watu wa kuigwa katika mchezo. Bruno yuko mbioni kuvunja rekodi na ametuvutia kwa kipaji chake. Bunny ni mshindi anayestahili. Ni chaguo bora na mchezaji bora.”