Bayern Munich macho kwa Martinelli

Muktasari:
- Na mabosi wa Arsenal wameripotiwa kuwa tayari kusikiliza na kupokea ofa zinazomhusu Mbrazili huyo.
MUNICH, UJERUMANI: BAYERN Munich imeonyesha dhamira ya dhati ya kunasa saini ya winga wa Arsenal, Gabriel Martinelli.
Na mabosi wa Arsenal wameripotiwa kuwa tayari kusikiliza na kupokea ofa zinazomhusu Mbrazili huyo.
Bayern inataka kuongeza staa mpya kwenye fowadi yao msimu huu na wanamtazama Martinelli kama mchezaji anayefiti vyema kwenye mipango yao.
Na kinachoripotiwa ni winga huyo mwenye umri wa miaka 24 ameanza kujadiliwa na mabosi wa Bayern kuona kama anaweza kufiti kwenye mipango yao ya msimu ujao.
Miamba hiyo ya soka ya Ujerumani inamfukuzia pia winga wa Athletic Bilbao, Nico Williams, licha ya kwamba Mhispaniola huyo anakaribia kwenda Barcelona.
Mastaa wawili wa Liverpool, Luis Diaz na Cody Gakpo nao wapo kwenye rada za miamba hiyo ya Allianz Arena, wakati winga wa Borussia Dortmund, Mwingereza Jamie Gittens kwenye mipango yao.
Arsenal inataka kupunguza bili yao ya mishahara na jambo hilo linaweza kushuhudia mastaa kadhaa wakafunguliwa mlango wa kutokea dirisha hilo la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Ripoti zinafichua Martinelli ni miongoni mwa wachezaji wanaoweza kufunguliwa mlango wa kutokea ikiwamo Oleksandr Zinchenko, Reiss Nelson, Jakub Kiwior, Fabio Vieira na Albert Sambi Lokonga.
Martinelli alijiunga na Arsenal akitokea Ituano kwa ada ya Pauni 5 milioni mwaka 2019. Tangu muda huo amecheza mechi 225 kwenye kikosi hicho cha Arsenal, amefunga mabao 51 na asisti 29. Mkataba wake huko Emirates utafika ukomo 2027 na Arsenal inahitaji ada ya Pauni 50 milioni kwenye mauzo yake.