Bado sana… Liverpool haijamaliza ishu ya Jota
Muktasari:
- Jota na kaka yake, Andre Silva, walifariki katika ajali ya gari huko Hispania wiki nne zilizopita, na tangu wakati huo, klabu imekuwa katika kipindi cha maombolezo.
LIVERPOOL, ENGLAND: BAADA ya kujitoa kwa namba mbalimbali ikiwamo kustaafisha jezi yake, mabosi wa Liverpool bado wameona haitoshi kumuenzi staa wao Diogo Jota na sasa wamepanga kufanya mambo kadhaa ambayo yataacha kumbukumbu yake daima.
Jota na kaka yake, Andre Silva, walifariki katika ajali ya gari huko Hispania wiki nne zilizopita, na tangu wakati huo, klabu imekuwa katika kipindi cha maombolezo.
Mashabiki kutoka sehemu mbalimbali duniani wamekuwa wakifika kutoa heshima zao kwa kuweka maua, jezi na jumbe za maandishi nje ya uwanja wa Anfield.
Lakini hiyo haijatosha kwa mabosi wa Liverpool, sasa wamekuja na mpango endelevu kwanza ni kujenga sanamu la mchezaji huyo nje ya Uwanja wa Anfield.
Hadi sasa jinsi sanamu hilo litakavyokuwa bado haijajulikana. Mbali ya sanamu hilo, Liverpool imepanga kupanda maua ya kumbukumbu katika maeneo yote ya klabu ikiwa ni pamoja na uwanja wa mazoezi na makao makuu ya timu ya wanawake.
Kama haitoshi, majogooo hawa wamepanga kuwepo kwa nembo ya ‘Forever 20’ (20 Milele) itakayochapishwa kwenye jezi mpya za msimu ujao za Liverpool zitakazotolewa na kuanza kuuzwa na adidas Agosti 1. Nembo hiyo itadumu kwa msimu mzima.
Zaidi ya hapo, ikiwa mashabiki watataka kuweka jina Diogo J na namba 20 nyuma ya jezi zao mpya, faida yote ya uchapishaji huo itapelekwa kwenye taasisi ya LFC Foundation ambayo ni sehemu ya Liverpool lakini yenyewe imekuwa ikihusika katika kusaidia jamii na watu wasiojiweza, hivyo pesa hizo zitatumika huko.
Taasisi hiyo ya Liverpool pia imeahidi kuanzisha mpango wa soka kwa ngazi ya jamii kwa jina la Diogo.
Katika mechi ya mwanzo wa msimu ujao kati ya majogoo hawa na Bournemouth itakayopigwa kawenye dimba la Anfield, Ijumaa ya Agosti 01, kutakuwa na picha kubwa ya Jota itakayochukua eneo kubwa la jukwaa pamoja na dakika moja ya ukimya kwa ajili ya kuomboleza kifo cha fundi huyu wa kimataifa wa Ureno ambaye msimu uliopita alikuwa msaada mkubwa wa Liverpool katika harakati zao za kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu England.