Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bado fainali za AFCON 2027 zimepoa

Muktasari:

  • Katika mazungumzo na baadhi ya rafiki zangu, wengine wa ndani ya CCM ambao hawakuwa na wazo la sababu zilizomsukuma Rais Samia kumteua mbunge huyo wa Arusha Mjini, niliwazindua nilipowaambia kuwa ameona mambo mengi ya ubunifu aliyoyafanya katika nafasi alizoshikilia awali, ikiwemo ya mkuu wa Mkoa wa Arusha.

WAKATI niliposikia Rais Samia Suluhu Hassan alipomteua Paul Makonda kuwa naibu waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, kitu kimoja kilikuja kichwani; fainali za soka za Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika mwakani nchini Tanzania, Kenya na Uganda.

Katika mazungumzo na baadhi ya rafiki zangu, wengine wa ndani ya CCM ambao hawakuwa na wazo la sababu zilizomsukuma Rais Samia kumteua mbunge huyo wa Arusha Mjini, niliwazindua nilipowaambia kuwa ameona mambo mengi ya ubunifu aliyoyafanya katika nafasi alizoshikilia awali, ikiwemo ya mkuu wa Mkoa wa Arusha.

Ni kweli, Makonda anazungumzwa kwa mengi, lakini ukiyaweka kando ukazungumzia mambo yanayoweza kuwa chanya kwake ni hilo la ubunifu na mikakati ya kutekeleza jambo lake.

Pengine hilo ndilo husababisha atuhumiwe katika mambo mengine, lakini kwenye hili la kupandishwa kuwa waziri kamili linaweza kuwa na uhusiano mkubwa na kuamsha wizara hiyo ili ishughulike kikamilifu na mambo yaliyo chini yake, hasa hili la uenyeji wa fainali zijazo za AFCON baada ya zile za ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) zilizofanyika katika nchi hizo tatu kutokuwa na msisimko wa ndani licha ya Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) kusema kuwa zilikuwa na mafanikio makubwa.

Na cheche zake tulishaanza kuziona, ingawa zinakumbana na ukosoaji fulani.

Waziri Makonda alimwalika nyota wa Afrika aliyetikisa soka barani Ulaya, Didier Drogba, wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake. Nadhani ilikuwa ni mara ya kwanza kwa mchezaji nyota wa Afrika aliyetamba barani Ulaya na kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika kuhudhuria kikao cha bajeti cha Bunge wakati wizara ikiwasilisha hotuba yake ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka unaofuata.

Ziara ya Drogba haikuwa na makandokando, lakini ile ya beki wa zamani wa Manchester United, Rio Ferdinand, ilikumbana na ukosoaji, labda kwa kuwa ilikuja wakati wizara imeshamaliza shughuli zake bungeni na hivyo wanaharakati kuichukulia kuwa ni mpango wa kufunika mambo ya kisiasa.

Hata hivyo, cha muhimu ni jinsi nyota hao walivyoweza kutikisa baadhi ya vyombo vya habari vya kimataifa licha ya mmoja wao kukosolewa sana. Ukosoaji wa ziara ya Rio ulibeba kutangazwa kwa Tanzania bila kuangalia mtazamo hasi uliohusishwa na ziara yake.

Kutumia watu maarufu wa klabu maarufu ni mbinu zinazotumiwa na taasisi nyingi kwa ajili ya kutangaza shughuli au bidhaa zake na ndiyo maana pamoja na matatizo yanayohusishwa na utawala wa Paul Kagame, bado Rwanda inatangazwa na klabu kubwa za soka duniani kama Arsenal na Paris Saint-Germain.

Hata CAF hualika nyota wa zamani kwenye fainali za mashi-ndano yake na hupewa ruhusa ya kuingia hata sehemu ambazo waheshimiwa hawaingii.

Ubunifu kama huu ulitakiwa uanzishwe na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) katika kutangaza fainali hizo za AFCON 2027 baada ya Serikali kutekeleza wajibu wake wa kutoa uhakikisho kwa CAF kuwa iko tayari kwa majukumu yote yanayoambatana na uenyeji wa fainali hizo kama usalama, miundombinu bora ya usafiri, michezo na malazi.

Na kama mdau mwingine amefanya ubunifu huo, ni jukumu la TFF kukumbatia na kupanua mkakati huo ili uchangie katika kusisimua fainali hizo za kwanza kufanyika katika ukanda huu wa Afrika Mashariki. Lakini ilionekana kama TFF ilikuwa nyuma kwenye ziara za wawili hao na ilichokuwa inasubiri ni mwaliko wa kuwepo kwenye shughuli za magwiji hao ambazo Serikali au waziri alipanga.

Ungetarajia moja ya vituo vikuu ambavyo nyota hao wangetembelea kuwa ni ofisi za soka na vituo vya ufundi ambavyo nyakati zote huwa na programu za mafunzo mbalimbali zinazoendelea, zikiwemo za makocha, watoto wadogo na nyinginezo, hivyo kujenga akilini mwao taswira ya kudumu ambayo inaweza kuwasukuma kufanya vizuri zaidi kufikia ndoto zao.

Inawezekana hakukuwa na uratibu mzuri, lakini si wakati wote baraka hushuka kama mvua kwa sababu Yakobo alizing’ang’ania usiku kucha hadi akabarikiwa alfajiri. Hivyo, ilikuwa ni jukumu la TFF kung’ang’ania kushirikishwa kwa kiwango kikubwa zaidi ili malejendari hao wawaachie baraka zao.

Kwa hiyo, kwa mara nyingine, sikushangaa wakati Waziri Makonda alipomtangaza Haji Manara kuwa msemaji wa timu zote za taifa na afanye kazi chini ya Baraza la Michezo la Taifa. Wengi wanazizungumzia zaidi timu za taifa za soka, lakini Haji anazagaa kote, yaani katika netiboli, kikapu, mikono, riadha na michezo mingine. Haji anajulikana kwa kuibua mijadala na kufuatiliwa na wengi. Kundi lake la WhatsApp la Footballers lina wafuasi wengi ambao huibua mijadala mbalimbali. Ni Ofisa Habari pekee aliyezitumikia klabu za Simba na Yanga kwa nyakati tofauti katika cheo hicho.

Anajulikana kwa kutengeneza rekodi na wasifu mzuri wa kitu anachokipigania na stadi nzuri ya kukiwasilisha kwa walaji. Mara kadhaa amekuwepo kwenye harakati hizo za kuipigania timu ya taifa na kwa wadhifa huo, anaweza kufanya vizuri zaidi kama wadau wote watampa ushirikiano anaoutaka. Mara kadhaa nimekuwa nikiandika kuwa hakuna hamasa inayotengenezwa kuelekea fainali hizo za AFCON 2027 kwa kuwa hata timu ya taifa haizungumziwi sana. Ni kama vile inaitwa, inacheza mechi nje ya nchi na baadaye kuvunja kambi.

Ule msisimko uliofanya Uwanja wa Benjamin Mkapa kujaa mashabiki waliovalia fulana za bluu umetoweka na hadi sasa ni nadra kujua kikosi cha kwanza cha Taifa Stars, achilia mbali vikosi vya michezo mingine.

Idara ya Habari na Mawasiliano ya TFF inajikita zaidi kutoa taarifa rasmi, tena kwa mtandao, bila kukaribisha mijadala ambayo huibua hisia za watu na kusababisha timu ya taifa iangaliwe sana.

Hakuna programu za waandishi wa habari na wachezaji wa Taifa Stars, hakuna programu za kocha kuwa na muda mrefu na waandishi kuhusu uteuzi wake na mkakati wake, wala kuzungumzia hali aliyoikuta.

Ni kama kocha wa sasa, Miguel Gamondi, ana mkakati wa kimiujiza ambao unaweza kufanya kazi bila kutegemea nguvu ya mashabiki na vyombo vya habari.

Bila mashabiki, wachambuzi na waandishi wa habari kuizungumzia timu yao, hamasa ya fainali za AFCON 2027 itakuwa ndogo na ufuatiliaji utakoma iwapo timu itatolewa mapema kama ilivyokuwa CHAN, tofauti na wenzetu wa Kenya na Uganda. Idara ya Habari na Mawasiliano ya TFF ina wajibu huo wa kutengeneza mkakati madhubuti wa mawasiliano kuelekea fainali za AFCON 2027 ili kuweka maana ya juhudi zote zilizotumika kuhakikisha nchi inakuwa mwenyeji wa mashindano hayo.

Kusubiri kutoa taarifa kwa waandishi kuhusu uteuzi wa timu, safari zake, uteuzi wa watumishi katika mechi za CAF pekee, hakuwezi kujenga taswira nzuri ya AFCON 2027. Kunahitajika kitu zaidi. Bila ya hivyo, fainali za AFCON 2027 zimepoa.