Aston Villa wanatambia kiwango cha Rashford
Muktasari:
- Rashford, 27, ameonyesha kiwango bora tangu alipojiunga na miamba hiyo ya Villa Park kwa mkopo akitamba chini ya kocha Unai Emery. Rashford bado hajafunga, lakini ameonyesha ubora akiasisti mara mbili.
BIRMINGHAM, ENGLAND: MASHABIKI wa Aston Villa wamemtaka bosi wa usajili wa timu hiyo kuhakikisha anamnasa jumla mshambuliaji wa Manchester United, Marcus Rashford, ambaye amejiunga kwa mkopo dirisha lililopita la majira ya baridi.
Rashford, 27, ameonyesha kiwango bora tangu alipojiunga na miamba hiyo ya Villa Park kwa mkopo akitamba chini ya kocha Unai Emery. Rashford bado hajafunga, lakini ameonyesha ubora akiasisti mara mbili.
Kiwango hicho cha Rashford kimekuja mwezi mmoja baada ya kocha wa Man United, Ruben Amorim kudai kwamba ni heri amuweka benchi kocha wa makipa, Jorge Vital kuliko kumpanga mshambuliaji huyo.
Amorim alisema kuhusu Rashford: “Ni heri nimuweke Vital kwenye benchi kuliko mchezaji ambaye haonyeshi ziada yoyote mazoezini kila siku. Siwezi kubadilika kwenye idara hiyo.
“Kila siku sababu ni ileile. Sababu ni mazoezi. Kwa namna ninavyomtazama mchezaji mazoezini, kwenye maisha yake kila siku. Kama mambo hayabadiliki, nami siwezi kuwa tofauti.” Mashabiki wa Aston Villa hawajasahau kauli hiyo ya Amorim na kumtaka bosi wa usajili kwenye timu yao, Monchi wakitania kwamba aende kumsajili Vital badala ya Rashford, ambaye anaonyesha mavitu ya maana kabisa kwenye kikosi chao kwa sasa.
Shabiki mmoja alitania kwenye mtandao wa X: “Kama Rashford ni mzuri kiasi hiki basi Monchi aende tu kumsajili kocha wa makipa wa Man United.”Shabiki mwingine alisema: “Anadhani huyo kocha atakuwa hatari zaidi.”