Ashley Young kukwaana na mwanaye Kombe la FA
Muktasari:
- Everton imepangwa kumenyana na Peterborough United kwenye Raundi ya Tatu ya Kombe la FA, uwanjani Goodison Park, Januari 11 mwakani.
LIVERPOOL, ENGLAND: STAA wa Everton, Ashley Young atakabiliana na mtoto wake wa miaka 18, Tyler kwenye michuano ya Kombe la FA.
Everton imepangwa kumenyana na Peterborough United kwenye Raundi ya Tatu ya Kombe la FA, uwanjani Goodison Park, Januari 11 mwakani.
Hiyo inamaana staa wa zamani wa Manchester United, Ashley, 39, atakwaana jino kwa jino na mtoto wake, ambaye anacheza kwenye League One akicheza kikosi cha Under-21 cha Petersborough.
Na Young amefurahia jambo hilo kupata nafasi ya kucheza dhidi ya mwanaye na kuamua kuandika kwenye ukurasa wake wa mitandao ya kijamii, akisema: "WOW……….Ndoto imekuwa kweli.#FaCup #Muda wa msisimko#YoungVsYoung."
Mashabiki nao wanasubiri kwa hamu kipute hicho kitakachokutanisha baba na mwana.
Shabiki wa kwanza aliandika kwenye mtandao wa X: "Natumai mtakabiliana! Hii ni ndoto kwenu! Nawatakia kila la heri!"
Mwingine aliandika: "Dabi ya familia ya Young."
Shabiki wa tatu aliandika: "Soka ipo spesho sana. Hii ni mechi ya aina yake!"
Shabiki mwingine alisema: "Hiyo ni safi. Natumaini itakwenda sawa kwenu nyote."
Na shabiki mwingine aliamua kwenda na hashtag: "#YoungvsOld."
Tyler alijiunga na Peterborough akitokea kwenye kikosi cha Under 18 cha Queens Park Rangers wakati wa dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya. Kiungo Tyler amecheza mechi moja tu kwenye kikosi cha wakubwa cha Posh katika mchezo wa EFL Trophy.
...