Arteta anavyotumia pesa nyingi kunasa Mastaa
Muktasari:
- Kama atanaswa, basi akitua Emirates atakwenda kukutana na wakali wengine kama Martin Zubimendi na Noni Madueke, ambao pia wamenaswa dirisha hili kwa pesa ndefu.
LONDON, ENGLAND: TOFAUTI kabisa na watangulizi wake, Mikel Arteta anapewa maisha yote ya kitajiri kwenye kikosi cha Arsenal, akipewa ruhusa ya kusajili staa yeyote kwa gharama yoyote.
Hilo linaweza kuthibitishwa kwa pesa iliyotumika kwenye usajili wa Arsenal tangu Mhispaniola huyo alipotua Emirates, kwamba ametumia robo tatu ya Pauni 1 bilioni kwenye usajili na sasa anakaribia kumnyakua straika wa kiwango cha dunia, Viktor Gyokeres. Arsenal inamtaka Gyokeres, ambaye amefunga mabao 97 kwa misimu miwili iliyopita huko kwenye soka la Ureno na kuhesabika kama moja ya straika tishio Ulaya.
Kama atanaswa, basi akitua Emirates atakwenda kukutana na wakali wengine kama Martin Zubimendi na Noni Madueke, ambao pia wamenaswa dirisha hili kwa pesa ndefu.
Baada ya kumaliza wa pili kwenye Ligi Kuu England kwa misimu mitatu iliyopita mfululizo, kocha Arteta ameamua kufungua pochi lake na kushusha mashine za maana, ambazo anaamini zitakuwa na nguvu ya kwenda kupambana na miamba mingine kwenye ligi.
Tangu alipotua kwenye kikosi cha Arsenal, Arteta ametumia Pauni 800 milioni kwenye usajili, huku akipewa maisha ya kitajiri ya kusajili na kutema kwa kadria anavyotaka.
Arteta ndiye aliyevunja rekodi ya uhamisho kwenye kikosi cha Arsenal alipofanya usajili wa kiungo Declan Rice kutoka West Ham United kwa uhamisho wa Pauni 105 milioni msimu wa 2023-2024. Alifanya pia usajili wa mastaa kadhaa kwa pesa ndefu katika harakati za kuifanya timu hiyo kuwa ya kushindania mataji.